Habari Mseto

Ukarabati wa barabara za lami waendelea Kiambu

May 19th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu inaendelea kuimarika kutokana na miundomsingi.

Katika maeneo mengi ya kaunti hiyo, ukarabati wa barabara kadhaa unaendelea.

Kwa muda wa wiki moja sasa wakazi wa kijiji cha Njiku eneo la manispaa ya Kikuyu wamepata afueni baada ya barabara ya umbali wa kilomita tatu kukarabatiwa katika eneo hilo.

Barabara hiyo ni ya Kanjiku-Kigothua ambayo inazidi kuendelea, hadi Limuru-Banana eneo la Riani ikifika hadi Ndenderu.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema ukarabati huo utaleta mabadiliko mengi ikiwemo kuimarisha biashara na usafiri.

“Kwa muda mrefu barabara hizo zimekuwa kero kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo. Lakini baada ya ukarabati huo wakazi wa maeneo hayo watanufaika pakubwa na kuendelea na shughuli zao bila shida,” alisema Dkt Nyoro.

Barabara hiyo itaunganisha eneo la Njiku-Kigithua hadi eneo la shule ya sekondari na ya msingi ya Muthurwa chini ya ufadhili wa Kenya Urban Support Project kwa ushirikiano na Kaunti ya Kiambu na Benki ya Dunia.

Alisema kwa zaidi ya miezi sita sasa Kaunti ya Kiambu imekarabati barabara kadhaa za mashinani katika eneo la Thika Mjini, Kiambu, na hata Limuru.

Bw James Kimani ambaye ni mfanyabiashara mjini Kikuyu anasema barabara hizo zikianza kutumika rasmi wafanyabiashara wengi pamoja na sekta ya usafiri itanufaika pakubwa.

“Kwa muda mrefu tumepitia hali magumu kwa sababu barabara nyingi zilikuwa zimejaa mashimo na wakati wa mvua matope yalikuwa mengi,” akasema Bw Kimani.

Naye Bw Peter Njuguna ambaye ni dereva wa matatu mjini Limuru anakiri magari yao yamekuwa yakikwama kwenye matope wakati wa mvua.

“Lakini sasa tunapongeza juhudi za Kaunti ya Kiambu kuwajali wakazi. Hayo ni maendeleo ya hali ya juu na tunapongeza juhudi zinazofanywa,” akasema Bw Njuguna.

Anaongeza pia ni fahari kubwa kwa Kaunti ya Kiambu kujenga upya kituo cha magari cha Limuru ambacho kilikuwa katika hali mbovu hapo awali.

“Wakati mwingi pahali pa kuegesha matatu ilikuwa ni shida huku magari mengi yakiegeshwa nje ya kituo hicho,” akasema Bw Njuguna.