Makala

UKATAJI MITI: Bei ghali ya mafuta inavyotishia misitu

September 8th, 2018 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

WAKATI serikali ilipopiga marufuku ukataji wa miti nchini, nia yake ilikuwa kulinda misitu, wanyama na vyanzo vya maji.

Naibu Rais William Ruto hapo Februari alifafanua kuwa ukataji miti ulikuwa unahujumu utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu kwani uharibifu wa mazingira ulikuwa unalemaza juhudi za kupata chakula cha kutosha kwa wananchi.

Lakini Wakenya wa tabaka la chini waliumia moja kwa moja kwa kuwa walikuwa wakitumia makaa kuandaa vyakula. Makaa yalipanda bei na kuwalazimisha kuanza kutegemea mafuta taa.

Wakati huo bei ya mafuta taa ilikuwa kati ya Sh66 na Sh75 kwa lita kwenye vituo vya mafuta, lakini baada ya ongezeko la ushuru kwa bidhaa za mafuta kwa asilimia 146 hivi majuzi, bei ya mafuta taa imechupa hadi Sh100 vituoni na Sh130 kwa lita madukani.

Taifa Jumapili ilizuru mitaa ya mabanda jijini Nairobi na kung’amua kuwa tangu marufuku ya ukataji miti ianze, wafanyabiashara wa makaa wamekuwa wakiagiza bidhaa hiyo kutoka mataifa jirani ya Sudan Kusini na Tanzania.

“Makaa hapa Kenya ni ghali sana na nadra kupatikana. Gunia moja ni Sh2,600. Sasa inatulazimu kununua kutoka kwa malori kutoka Sudan Kusini ambayo hutuuzia kwa Sh1,900 kwa gunia. Malori ya Tanzania hutuletea kwa Sh2,100 kila Jumatano,” akasema Mary Wanjiru, ambaye ni mama wa watoto wawili mtaani Uthiru.

Hata hivyo, bei ya makaa ni ghali kwa watumizi wake. “Ninanunua makaa mkebe mmoja kwa Sh60 lakini nitapika chakula cha mchana pekee. Wakati mafuta taa yalikuwa bei nafuu, ningepika mara nne nikitumia lita moja ya Sh70,” akasema mkazi mmoja jijini ambaye hakutaka kutajwa.

Bei hii ghali huenda ikachochea baadhi ya wananchi kuamua kuvunja sheria ya ukataji miti wakijitetea kuwa kuni ndiyo suluhu iliyosalia kwao kujiepusha na gharama ya juu ya maisha.

Lakini mtaalamu wa mazingira na afisa katika Chama cha Walinda Misitu nchini (FSK), Bi Carole Wanjiku anashauri kwamba kuna mbinu mbadala za kupika ambazo gharama yake iko chini ikilinganisha na gesi, makaa au mafuta taa.

Mkazi wa mtaa wa Uthiru, Nairobi apasua kuni. Watumizi wengi wa wa makaa sasa wamegeukia kuni baada ya bei ya mafuta taa kupanda. Picha/ Faustine Ngila

“Kuna teknolojia za kutengeneza makaa ya bei nafuu kwa kutumia maramba (sawdust), karatasi kuukuu na pia mianzi (bamboo). Kauna baadhi ya kampuni zinazoshirikiana na serikali kuongeza muda wa kudumu wa makaa hayo kama Bidco Ltd,” anasema.

Mtaalamu huyo anaelezea kuwa makaa ya kawaida hayawezi kutumika kwa muda mrefu na mbinu bora ni kuondoa kiwango cha Carbon kiteknolojia ili kuongezea muda wa matumizi.

Ingawa baadhi ya wakazi mijini wamelemewa na bei ghali ya makaa na kugeukia kuni, hiyo si suluhu ya siku za usoni kwani kuni hizo zitaisha.

“Kuna miradi nchini ya kutoa suluhu tosha kwa tatizo hili. Mradi wa kuwapa wakulima fursa ya kupanda miti yao wenyewe na kukata matawi pekee kuunda gesi ya kupikia (biogas) na pia kuni ndizo suluhu tosha kwa miaka ijayo,” anasema Bi Wanjiku.

Katika miradi hii, wakulima hupewa miche ya miti ambayo wanapanda kwa manufaa ya siku za usoni.

Lakini ni suluhu ipi inaweza kutumika kila sehemu ya nchi kwa gharama ya chini zaidi kwa sasa?

“Kuna uchafu mwingi nchini kutokana na kinyesi cha mifugo na wanyama ambacho kinaweza kutumiwa kuunda gesi ya kupikia.”

Pia mradi wa mianzi kuunda gesi hii utasaidia pakubwa kuokoa Wakenya kutokana na bei ghali ya mafuta taa, gesi na makaa huku tukihifadhi mazingira.”