WANDERI KAMAU: Ukatili kwa wanahabari ni dalili za enzi za giza

WANDERI KAMAU: Ukatili kwa wanahabari ni dalili za enzi za giza

Na WANDERI KAMAU

WAKATI wa harakati za kupigania ukombozi wa kisiasa nchini katika miaka ya sabini, themanini na tisini, moja ya mbinu kuu ambazo utawala wa Kanu ulitumia ni kuwanyamazisha wakosoaji wake.

Nyakati hizo, makundi yaliyoonekana kuwa “maadui” wa serikali ni wasomi, mawakili, wanahabari na watetezi wa haki za binadamu.

Hivyo, serikali za marehemu Mzee Jomo Kenyatta na Daniel Moi zilifanya kila ziwezalo kuyanyamazisha makundi hayo—bila kuogopa lolote.

Fasiri kuu ya “kunyamazishwa” katika nyakati hizo ilihofiwa na wengi. Haikumaanisha kuwekewa vikwazo vya kutozungumza—bali kutekwa nyara au hata kuuawa.

Kuna mifano mingi ya wanasiasa, wasomi na wanaharakati waliouawa kikatili kutokana na ukosoaji wao mkubwa dhidi ya tawala hizo.

Sababu kuu ya urejeleo huu mchungu ni mtindo mpya ambao umeibuka katika siku za hivi karibuni, ambapo wanahabari wamekuwa wakishambuliwa au kupatikana wameuawa katika hali tatanishi, bila majibu kutolewa na idara kuu za usalama nchini.

Mnamo Novemba 14, mwandishi wa habari Mwangi Muiruri wa shirika la Nation Media Group (NMG), alishambuliwa na kuhangaishwa na watu wanaoaminika kuwa walinzi wa Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Alhamisi, mwili wa mwanahabari mkongwe Gatonye Gathura ulipatikana katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha, kaunti ya Nakuru, baada ya kutoweka kwa karibu mwezi mmoja.

Cha kushangaza ni kuwa, polisi walisema mwili huo ulipatikana ukiwa umetupwa katika eneo la Kihooto (Naivasha) Oktoba 26! Hilo linamaanisha mwili huo ulikuwa umekaa katika mochari hiyo kwa muda wa mwezi mzima bila yeyote kuutambua.

Hata kabla ya maombolezo ya mwendazake Gathura kuanza, tasnia ya uanahabari iligongwa na dhoruba jingine. Mwili wa mchoraji vibonzo Joshua Nanjero wa gazeti la ‘Nairobian’ linalomilikiwa na shirika la Standard Group, ulipatikana katika nyumba yake jijini Nairobi.

Bila shaka, visa hivyo ni vya kutia hofu, hasa wakati huu kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 zinaendelea kushika kasi.

Ingawa makala haya hayalengi kuwatakasa wanahabari hao, suala linazozua wasiwasi ni kimya cha serikali na idara za usalama kuhusu masaibu yaliyowafika.

Historia imeonyesha kuwa moja ya mbinu ambazo tawala za kiimla duniani hufanya ni kuvihangaisha vyombo vya habari, wakati zinapoanza kuhujumu na kuvuruga demokrasia.

Je, hizi ni dalili za hatari nchini?

akamau@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Biashara haramu ya Titi (sehemu 3)

Mbunge akanusha kuhamia UDA

T L