BAHARI YA MAPENZI: Ukatili wa kijinsia ni suala la kimamlaka

BAHARI YA MAPENZI: Ukatili wa kijinsia ni suala la kimamlaka

HIVI karibuni nilipita kwenye soko moja maarufu mjini Mombasa na katika shughuli zangu nilikutana na msichana ambaye alionekana ana ulemavu wa akili na pia mjamzito. Hiyo haikuwa hoja.

Jambo lililonifanya nisimame na kuangalia tena mara ya pili ni maneno yaliyokuwa yanasemwa na baadhi ya wauzaji na wabeba mizigo katika soko lile.

Kwamba inakuwaje mwanamke ambaye ni mlemavu wa akili anakuwa mjamzito. Kuna mwingine akasema alibakwa, wakati mwingine akisema ni hiari yake.

Nikatafakari mno iwapo kweli alifanya tendo lile kwa hiari yake au aliyeamua kushiriki naye kimapenzi alitumia nafasi kwamba ana ulemavu wa kiakili kumkatili kijinsia!

Iwapo wewe ni msichana, kijana, mwanamke ama mwanaume, bado unaishi na familia yenu ama umeanza uhusiano wa kimapenzi ama ndoa, bila shaka umewahi kukutana na tukio ambalo lilikukosesha amani, kukudhalilisha ama kuvunja moyo wako.

Kwa ujumla, ukatili wa kijinsia, hasa ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni matokeo ya tofauti ya hali ya mahusiano ya kimamlaka kati ya mwanamke na mwanaume katika familia na jamii.

Hali hii tofauti kwa upande mwingine hubebwa na mfumo wa sheria, malezi na makuzi na hata tofauti katika kupata na kumiliki raslimali mbalimbali.

Pia ukatili huu hadaa kwa wanawake na wasichana ni matokeo ya kuhalalishwa kwa vitendo vya kikatili kwa kisingizio cha hatua za kinidhamu ndani ya mamlaka na madaraja ya kijamii pamoja na makundi rika.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba vitendo hivi hufanywa na watu ambao tumewazoea, tunaoishi nao kila siku na huenda ambao tunawaamini na kuwategemea.

Kuongezea na hivyo ni kwamba wengi wanaotendewa baadhi ya vitendo hivi hawatambui kwamba wanaonyanyaswa na wengine wanaweza kuwa wanatambua lakini wanaamua kutochukua hatua yoyote na kuendelea katika hali hatarishi ambayo wakati mwingine hufikia tamati kwa kifo.

Takwimu za dunia zilizotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba katika kila wanawake watatu, mmoja ni muathirika wa ukatili wa kijinsia na hapa Kenya asilimia 45 ya waathirika ni wanawake na wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49.

Halikadhalika, kati ya wanawake watano nchini Kenya, mwanamke mmoja amekeketwa, wakati asilimia 23 ya wasichana wote nchini wameolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18.

Kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Covid 19, hali imeripotiwa kuwa mbaya zaidi.

Kuna ukatili unaoendana na vitendo vya vitisho ili mhusika aweze kupata huduma anayohitaji.

Aina hii hufanyika wakati mtu anayefanya kitendo hicho anachukua fursa ya nafasi yake ya ukuu kuomba upendeleo wa kijinsia.

Mhasiriwa anatishiwa kutekeleza vitendo hivi kinyume na mapenzi yao. Huwa ikijitokeza mara kwa mara mahali pa kazi, lakini pia kielimu.

Ukatili wa kingono ambapo mnyanyasaji anatumia udanganyifu na kulazimisha, kama ilivyo kwa watoto au watu wenye ulemavu.

Kupendeza, kupendekezwa wazi kwa maneno, na kupenya ni sehemu ya unyanyasaji wa kijinsia.

Hata hivyo vitendo hivi huwaathiri zaidi wasichana na wanawake kuliko wanaume na mara nyingi athari kubwa huwapata walio katika kundi hilo.

sizarinah@gmail.com

NA ifahamike kwamba ukatili wa jinsia ni ukiukaji wa haki za kimsingi za binadamu.

Si mke si mume. Lazima jamii na familia zichukue hatua za dharura kutambua, kuhamasisha umma, kuzuia na kuharamisha ukatili wa aina zote. Serikali na sekta binafsi zina wajibu kuchangia pakubwa katika uhamasishaji umma na kuzuia visa vya ukatili wa jinsia.

Hakuna upendo kwenye familia zisizothamini heshima. Wala hakuna haja kuhimiza watu kuoana iwapo hawajui maana halisi ya wawili kuwa mwili moja.

Haja gani kutia chudi watoto kuwasaka ikiwa wazazi hawana haja kudhihiri heshima na kudumisha hadhi ya watu wazima?

Ukatili wa kijinsia unaathiri misingi na uthabiti wa familia. Tunaposoma asili ya binadamu kutoka kwenye Vitabu Vitakatifu, manthari inayokita akilini ni ile ya ushirika na upendo. Mwanamume na mwanamke walikusudiwa kuwa wamoja wanaoshiriki mwili, akili na nafsi moja.

Walikusudiwa kufaana licha ya kuwepo tofauti baina yao.

Je, vita ni vya nini katika maisha ya watu walioumbwa kufaana?

Tunaweza kukariri ukweli kwamba ukatili wa kijinsia ni moja kati ya visa vya ukiukaji wa madhumuni ya Muumba.

Tumesikia visa vya wanaume wafidhuli wanaopiga na kuwajeruhi wanawake kila uchao.

Gumegume hawa wameshikilia ile dhana potovu kwamba mke yuko chini ya mumewe hivyo anaweza kupokezwa bakora kwa raha ya mwanamume.

Hebu nifahamisheni nyie mnaopiga wanawake. Kosa gani linalostahili adhabu ya bakora ama magumi usoni?

Je, nani asiyekosa kwa namna moja ama nyingine awe wa kwanza kufumbata konzi?

Mwanamume akijua vyema hadhi yake hana haja wala sababu kumpiga mwanamke mangumi usoni ama popote mwilini mwake.

Kama hayawani wanasuluhisha tofauti zao bila kuchaniana ngozi sembuse binadamu wenye tathmini na akili?

Falsafa ya nani yuko juu ama chini ya mwingine sio muhimu katika maisha ya wangwana wanaojua asili ya binadamu.

Nijuavyo ni kwamba aliye juu kawekwa juu kudhihiri uongozi na unyoofu. Alikusudiwa kuwa mfano mwema, kiongozi mwenye hadhi na heshima wala sio bahaluli mwenye kuwadhalilisha wafuasi walio chini.

Ithibati ya kuwa juu ni kudhihiri akili razini, wanyonge kuwapa sauti wala sio kuwakandamiza nyayoni.

Heshima ya kuwa juu ni kusuluhisha tofauti kwa unyenyekevu huku kila mmoja akitoa mchango kuhuisha na kudumisha upendo.Japo visa ni vichache, lakini wako vilevile wanaume wanaotandikwa na kuadhibiwa na wanawake waliokwisha sahau heshima na hadhi ya mwanamke kamili.

Aidha ukatili wa jinsia sio vita vya nyumbani pekee, kuna waliokataa katakata kumpa mwanamke uhuru wa kujieleza, kujiamulia na kudhihiri chaguo lake?

Eti mke hawezi kuvalia anavyotaka wanasema mahambe wanaosisimka mili wanapoona nyonga za kike! Ndio hao wanaolindwa na jamii eti. Sijui nani mkuu wa jamii mwenye kutunga hizi “sheria” zilizopitwa na wakati!

Ungwana katika maisha ni wepesi kukubali mazito na kuyachukulia vyema na wenzio. Mengi wanayobeba wenzetu daima yanaweza kuwa nanga kwetu.

Nasema kwetu kwa maana ya akina sisi tuliojaaliwa ila hatuna jaala.

Hakuna nafasi ya mwanamume jeuri ama mwanamke fidhuli. Ama ule msemo wa mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu haujakita akilini?

obene.amuku@gmail.com

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Je, kuwapa watoto uhuru ni kuwaharibu?

KPA yatikisa tena kwa kuilemea Don bosco TZ

T L