Pambo

Ukiachia mjakazi shughuli zote nyumbani utakuja kulia kunyang’anywa mume

April 28th, 2024 2 min read

NA WINNIE ONYANDO

JUMA lililopita nikiwa ndani ya matatu nikielekea nyumbani, niliketi kando ya wanawake wawili.

Nilipowatupia jicho, walionekana kuwa watu ambao wamedumu kwenye ndoa na kuelewa masuala ya ndoa.

Safari ilipoanza, wawili hao walianza gumzo lililoninasa nikawa nimetega sikio nisikilize maana walikuwa na mengi ya kusema.

Walizungumzia mambo mengi ila nikavutiwa makini na suala la kuajiri mjakazi.

Kati ya wawili hao, mmoja alidai kuwa hawezi kuajiri mjakazi kwani anaelewa sababu za mumewe kumuoa.

“Mimi siwezi kuajiri mjakazi. Ndio anyakue mume wangu? Siwezi hata kidogo. Nafanya kila kitu nyumbani hivyo, sioni haja ya kuwa na mjakazi,” mmoja huyo alijieleza.

Hata hivyo, mwenzake alinishangaza mno.

Alisema kuwa hawezi kukaa bila mjakazi kwake.

“Kwetu sisi tulilelewa na mjakazi. Alikuwa akifanya kila kitu. Hivyo sijazoea kufanya kazi. Hii ndio mama siwezi kukaa bila mjakazi kwangu,” akasema.

Kando na hayo, nilimsikia akisema kwamba tangu aolewe 2015, hajawahi kukaa bila mjakazi.

“Niliajiri mjakazi pindi tu nilipoolewa. Siwezi kujitesa. Niende kazi kisha tena nirudi nyumbani kung’ang’ana na kazi ya nyumba? Hiyo sahau,” akasema.

Kwake, mjakazi hufanya kila kitu ikijumuisha kutandika kitanda chao.

Kadhalika, mjakazi humshughulikia mume wake na hapa alimaanisha kumpikia, kumpigia nguo pasi, kumpelekea maji ya kuoga bafuni miongoni mwa kazi nyingine.

“Kwani kazi yake ni gani (mjakazi)? Namlipa afanye hizo zote.”

Nilivyomuelewa mwanamke huyo, kwake hakuna haja ya kuteseka yaani, kurauka kazini kisha kurudi nyumbani na kuanza kung’ang’ana na mwanamume ilhali ana mjakazi.

Gumzo likawa limenoga ila wakawasili walikokuwa wanaenda na kushuka huku wakiniacha na maswali tele.

Naelewa kwamba mwanamke huwa na kazi nyingi hasa pale ambapo anapopata mtoto.

Hii ndio maana wengi huajiri mjakazi ili hata naye aweze kupumzika.

Hata hivyo, ni hatari kumtwika mjakazi jukumu la kumshughulikia mume wako.

Mume wako alikuoa, hakumuoa mjakazi.

Hivyo hata kama umechoka kiasi gani, ni jukumu lako kama mwanamke kutekeleza majukumu yako ya ndoa.

Katika ndoa ni muhimu angalau kumtimizia mume mahitaji na kuona pia anakuwa nadhifu.

Mwanamume ataka kudekezwa na unapoachia mjakazi nafasi hii, huenda ukahatarisha ndoa yako. Hii ni kwa sababu wanakuwa na uhusiano wa karibu, hali ambayo huenda ikaanza kujenga hisia za kimapenzi kati yao.

Si makosa kwa mke kupata usaidizi wa shughuli za nyumbani kutoka kwa mjakazi wake. Hata hivyo, lazima ajuwe kuweka mipaka ambayo itasaidia kudumisha heshima kati ya wahusika wote na kulinda ndoa.

Kitabu kitakatifu kinatukumbusha kuwa, mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, lakini mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.