Ukikutana na hizi ‘kanda mbili’ utajua ni za sungura?

Ukikutana na hizi ‘kanda mbili’ utajua ni za sungura?

Na SAMMY WAWERU

IKIWA imeorodheshwa kati ya nyama nyeupe, ambayo ni mwororo na yenye ladha tamu, ni nadra kuipata kwenye hoteli au mikahawa.

Si nyingine ila ni nyama ya sungura. Bado haijakumbatiwa kikamilifu, licha ya manufaa yake chungu nzima kiafya na virutubisho.

Kwa wafugaji wa wanyama hao maridadi wa nyumbani, kupata soko haijakuwa mteremko.

Hata hivyo, Millimag Rabbits Farm, mradi ulioasisiwa na barobaro mmoja Pwani ya Kenya, umegundua siri kupenyeza mazao ya sungura sokoni.

Ukiwa ulijiunga na safari ya uzalishaji wa wanyama hao miaka mitano iliyopita, mradi huo ulioko eneo la Bamburi, Kaunti ya Mombasa, huongeza nyama thamani.

Hutengeneza soseji na bunny burger kwa kutumia nyama za sungura, hatua ambayo kulingana na Justin Magiri, mwanzilishi, imemsaidia kwa kiasi kikubwa kunenepesha mabawa ya soko.

Millimag Rabbits Farm, ina buchari – kichinjio cha kisasa, na ambacho kinaafikia vigezo vya haki za kimataifa kuhusu wanyama, kwa mujibu wa sheria za World Animal Protection, shirika lisilo la kiserikali (NGO) linalotetea maslahi ya wanyamapori na wa nyumbani.

“Tuna mashine za kisasa, zinazotumia nguvu za umeme kuchinja sungura, pasi kuwapitishia uchungu usiomithilika,” Magiri asema.

“Mifugo inapochinjwa kwa njia zinazoifanya kuhisi uchungu kupita kiasi, bila kuzingatia haki zao, hutoa homoni zinazoathiri ubora wa nyama,” Dkt Victor Yamo, Meneja anayeendesha kampeni kutetea haki za wanyama katika World Animal Protection, atahadharisha.

Baada ya kuchinja sungura, Magiri anasema huwaning’iniza ili damu kutiririka na kuondoa inayosalia, na vilevile kutoa ngozi.

Shughuli hiyo huendelezwa kati ya saa 12 – 24 kuondoa maji, kabla kutoa mifupa.

“Mifupa inapoondolewa, husaga nyama tayari kuongeza thamani,” adokeza.

Kulingana na Magiri, soseji na burger huzisindika kwa kutumia viungoasilia kama vile Parsley na Rosemary.

Nyama zilizosagwa na viungo hivyo, huchanganywa kwa kutumia maji, kisha zinablendiwa pamoja.

“Soseji tuna mashine (filler) ya kuzitengeneza, na hutumia matumbo ya kondoo (large intestines) mahala pa umbo,” mjasirimali huyo aelezea.

Matumbo ya mbuzi yametajwa kuwa bora zaidi katika utengenezaji wa soseji.

Millimag Rabbits Farm ilikumbatia mfumo wa kuongeza nyama za sungura thamani 2019, na Magiri anasema hupakia bidhaa kwa kipimo cha gramu 500 na kilo moja.

Aidha, kilo moja ya nyama ya sungura huuza Sh750, paketi ya soseji 8 Sh300 na gramu 400 za burger Sh400.

Mmoja wa wafanyakazi wa Justin Magiri (kulia), anayemiliki mradi wa Millimag Rabbits Farm, ulioko Bamburi, Mombasa, akionjesha baadhi ya waliohudhuria maonyesho ya nyama, Nairobi KICC Meat Expo, nyama za sungura. PICHA | SAMMY WAWERU

Mbali na kuongeza nyama thamani, mradi huo hutumia ngozi za sungura kuunda viatu maridadi (mocky shoes) na pia kandambili.

Isitoshe, hutengeneza mifuko, mazulia na mikeka.

“Mkojo wa sungura na kinyesi, hutumia kuunda mboleaasilia na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa,” Magiri asema, akiongeza kuwa wana mpango wanaoendeleza kusambaza bidhaa hiyo kwa vituo vya watoto yatima bila malipo, kufanya kilimo.

Millimag Farm kwa sasa ina sungura wapatao 385, wa kujamiisha na kuzalisha, ambapo ina mkataba wa makubaliano-kandarasi na wakulima wafugaji.

Magiri anaiambia Akilimali kwamba wanashirikiana na vijana na makundi matano ya kina mama katika ufugaji wa sungura.

Huwauzia vitungule (wana wa sungura), kuendeleza uzalishaji, wanapokomaa mradi huo unawanunua.

Kitungule mmoja hugharimu kati ya Sh1,000 – 1, 500, sungura wa kiume aliyekomaa Sh4, 000 na kike Sh3, 000.

“Janga la Covid-19 limeturejesha nyuma sana. Kufikia mwanzoni mwa mwaka uliopita, 2020, tulikuwa na sungura 800 wa kujamiisha na kuzalisha,” asema, akikadiria athari za corona katika mchango wao mkuu kuzalisha nyama za sungura nchini.

Anasema walilazimika kupunguza idadi hiyo, kwa sababu ya soko kuathirika na bei ya chakula cha madukani kupanda.

Sungura hulishwa chakula maalum aina ya pellets na nyasi za hay.

Mfugaji huyu hata hivyo ana imani taifa na ulimwengu litashinda vita dhidi ya janga hili la kimataifa, ambalo limekuwa kero kwa ukuaji wa uchumi wa nchi nyingi, Kenya ikiwemo.

Millimag Rabbits Farm inajivunia kuwa miongoni mwa wakulima na wafugaji walioshiriki maonyesho ya siku mbili ya nyama, Nairobi KICC Meat Expo.

Maonyesho hayo ya Novemba 18 na 19, yenye mada Safe and Quality Meat for Nutrition, Health and Wealth Creation, yaliandaliwa na Shirika la Nation Media Group Plc (NMG), kwa ushirikiano na serikali ya Kenya kupitia Idara ya Mifugo (SDL), Kenya Markets Trust (KMT), The Retail Trade Association of Kenya (RETRAK), na Meat and Livestock Exporters Industry Council of Kenya (KEMLEIC).

You can share this post!

KIPUTE CHA TIM WANYONYI: Leads United inapigiwa chapuo...

Nafasi finyu mjini lakini ufugaji mbuzi umenawiri si haba

T L