Makala

Ukimnong’onezea mkeo maneno matamu, atakutambua kama simba wake

Na BENSON MATHEKA August 13th, 2024 2 min read

MKE si wa kugombezwa, kukaripiwa na kufokewa. Hapana.

Ukifanya hivi unamsukuma mbali nawe kaka. Mke ni wa kuzungumziwa kwa upole, kwa maneno teule ya kumliwaza, maneno ya kumchangamsha na kuonyesha unamjali.

Badala ya kumngurumia mkeo akuogope kama simba, mnong’onezee maneno matamu ya kuongoa na atakutambua kama simba wake.

Maneno ya kumsifu na kumpongeza. Mwegemee sikioni na umwambie anaonekana mrembo.

Akivaa mavazi yanayomchukua vyema mwambie, “Mamii unavutia ajabu”.

Hii itamfanya ajue unamtambua na kumpenda alivyo na hakukosea kukufanya chaguo la mpenzi wake.

Usisubiri aambiwe na wanaume wengine. Kuwa wa kwanza awe akiwaambia mume wangu alitambua hilo au ikiwa inampendeza mume wangu, niko sawa.

Sikia kaka, usimlaumu mkeo kila wakati kwa malezi ya watoto. Mmiminie sifa sikioni mwake.

Mkaribie na umwambie ni mama wa ajabu mkiwa kwenye watu. Hakuna kinachomfanya mwanamke kufurahi kama kusikia baba wa watoto wake akithamini jinsi anavyowalea.

Mkiwa wawili kwenye hafla kuliko na watu wengi, usilazimishe mkeo kuondoka. Mkaribie sikioni na kumwambia afadhali muondoke mwende nyumbani kuwa wawili.

Kuna siri hapa; Mwanamke hupenda kuwa na mumewe tu wakifanya na kupanga mambo yao.

Kumbuka, usimkaripie, mnong’onezee haya na utamuweza na akitabasamu, usikose kutambua na kumwambia pale pale sikioni unapenda tabasamu lake.

Hili linatosha kuongezea mkeo bidii, upendo na miaka ya kuishi katika ulimwengu huu.

Kwa kufanya hivi, atakuhudumia vyema zaidi. Mpe mkeo sababu ya kuona fahari ya kukuchagua kama mume.

Kumwambia mambo mazuri kutamfanya atabasamu zaidi na furaha itakuwa kwako kaka.

Wakati mwingine mkaribie mkeo kumnong’oneza sala sikioni. Mazungumzo kati ya watatu; yeye, Mungu na wewe.

Mwanamke hupenda kuombewa na mumewe. Sikia kaka, mkeo akichukua muda kukupikia chakula kizuri, mpongeze. Usijaze tumbo na kujilaza bila kumshukuru.

Kuna wanaume wanaotamani kuwa na mke anayejua kupika.

Mtie shime mke kama huyo na utaona matunda ya hatua yako.

Onyo: Hakuna mwanamke anayepikia mume anayewajibika na kujukumika vilivyo chakula kibaya kwa kuwa huwa anauliza bwanake anachotaka kula.

Wanawake wanapenda kutafutwa.

Unapomfeel mkeo, mkaribie sikioni na umwambie kuwa unamtamani kwa dharura. Isiwe ni masuala ya chumbani na mezani pekee.

Mlinde mkeo kwa kila hali na hatari kaka.

Ukiona jambo linaloweza kumuaibisha hadharani, mlinde dhidi ya aibu, mnong’oneze. Iwe ni vipodozi kufutika na kuchafuka, mjulishe kwa nong’onezo. Inamhakikishia kuwa ana dume linalomjali, kumlinda na kumkinga kwa hali zozote.

Mwanamke hachoki kuhakikishiwa kwamba anapendwa. Mpende mkeo kwa maneno na vitendo.

Mkeo ni ua lako na hivyo basi ni jukumu lako kaka kulimwagilia maji kwa maneno ya kumfanya aamini unamthamini.