Ukimwi: Kaunti zalaumu umaskini na dhuluma za kijinsia, ngono
OSBORN MANYENGO Na DAVID MUCHUI
KAUNTI ya Trans-Nzoia imerekodi ongezeko la asilimia 1.6 ya maambukizi mapya ya ya virusi vya ukimwi chini ya mwaka mmoja uliopita umaskini na mimba za mapema zikilaumiwa.
Kwa mujibu wa Naibu Gavana Kaunti ya Trans-Nzoia, Bi Bineah Kapkori, umaskini na ukosefu wa mahitaji muhimu kwa wasichana umepelekea ongezeko la mimba za mapema zinazohusishwa na mambukizi hayo.
Akihutubia umma katika uwanja wa Maili Saba Kaunti ndogo ya Kwanza, Trans-Nzoia kwenye hafla ya kuadhimisha siku ya Ukimwi duniani, Bi Kapkori alisema serikali ya Kaunti chini ya Gavana George Natembeya iko mbioni kuhakikisha sekta ya afya imenawiri kwa kuweka dawa na wahudumu wa kutosha katika kila kituo cha afya cha umma.
Naye mratibu wa Ukimwi katika Kaunti ya Meru Joseph Murungi alisema maambukizi mapya miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 25 yameongezeka miaka ya hivi karibuni.
Bw Murungi alisema rekodi za idara ya afya zinaonyesha kuwa dhuluma za kimwili, kingono na kisaikolojia zimekithiri.
“Kulingana na rekodi zetu, kati ya wale wanaoripoti dhuluma za kimwili, idadi kubwa ya watu huwa na vidoda vinavyotokana na kuumwa. Inaonekana wakazi wa Meru ni wepesi wa kuumana,” Bw Murungi alisema.
Next article
Kirui kivutio Fukuoka Marathon Japan, aendea taji la Githae