Habari Mseto

Ukisema ‘mtu mmoja, kura moja, shilingi moja’, nasi tutasema ‘kilomita moja’, Gachagua aambiwa

May 21st, 2024 1 min read

NA MUMBI WAINAINA

VIONGOZI kutoka maeneo kame wamemkosoa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa wito wa kuwapa watu pesa za maendeleo kulingana na idadi yao, wakisema siasa hiyo haina nafasi nchini.

Wakizungumza katika hoteli ya Serena, Nairobi Jumanne, viongozi kutoka kaunti 13 walisema maeneo mengi kame ni makubwa. Kwa hivyo wito wa Bw Gachagua utazuia maendeleo katika maeneo hayo.

Mbunge wa zamani wa Tiaty, Bw Asman Kamama alisema mkakati huo utatumika kuibia Wakenya.

“Wale wanaotangaza maneno haya wanadhani hatujaenda shule. Huu nii ufisadi kupitia mlango wa nyuma. Unataka kuiba rasilimali kupitia sera. Sera hio ndiyo tunayokataa kikamilifu,” akasema Bw Kamama.

Walisema maeneo yao yako na idadi kubwa ya watu ila wengi wao hawana vitambulisho. Hivyo wakati wa chaguzi hawana uwezo wa kupiga kura.

Taarifa iliyosomwa na aliyekwa Spika wa Seneti, Bw Ekwee Ethuro, ilisisitiza umuhimu wa kutambua kwamba ufugaji katika eneo kame unachangia pakubwa katika uchumi wa nchi.

“Pia tutapigania mkakati wa mtu mmoja, kura moja, kilomita moja katika ugavi wa rasilimali,” akasema Bw Ethuro.

Viongozi hao wanatoka kaunti za Mandera, Wajir, Garissa, Marsabit, Isiolo na Turkana. Nyingine ni Samburu, Baringo, West Pokot, Tana River, Kajiado, Narok na Lamu.

Aliyekuwa gavana wa Kaunti ya Garissa, Bw Ali Korane alisema, “Kati mwa Kenya ni sehemu ndogo sana ya nchi, kwa kuiweka katika muktadha. Kanda hio ya kati ni kilomita za mraba 13, 121, yenye lami ya kilomita 7,000 kati ya kilomita 18,000 za nchi zenye barabara ya lami. Jimbo la North Horr lenye kilomita za mraba 38,954 za ardhi hazina hata sentimita moja ya lami barabarani.”