Ukitapeliwa pesa kwa simu ni heri uzisahau tu – DCI

Ukitapeliwa pesa kwa simu ni heri uzisahau tu – DCI

Na LEONARD ONYANGO

UWEZEKANO wa kurudishiwa fedha zako baada ya kutapeliwa na wahalifu kwa njia simu au mtandao, ni mfinyu, polisi wameonya.

Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) jana ilikiri wahalifu wanaotapeli watu fedha kwa njia ya simu au mitandaoni ni vigumu kuwanasa kwani wanatumia laini na vitambulisho vya watu wengine.

Idara ya DCI inayoongozwa na George Kinoti, jana ilionya Wakenya dhidi ya kulipa fedha kwa njia ya simu au mitandao kwa kampuni, mashirika au watu wanaotiliwa shaka.

DCI ilisema kuwa kumekuwa na ongezeko la visa ambapo wahalifu wamekuwa wakitapeli vijana kwa njia ya simu au mtandaoni kwa ahadi ya kuwasaidia kupata ajira humu nchini na ughaibuni.Idara ya DCI pia ilionya wananchi dhidi ya kununua bidhaa mitandaoni na kukodisha magari kupitia mitandao.

“Lakini watu hao wakishalipwa fedha wanatoweka na ni vigumu kuwapata,” akasema Bw Kinoti.“Baadhi ya walaghai wanatumia picha za watu maarufu katika akaunti zao za mitandao ya kijamii wanazotumia kutapeli watu,” akasema Bw Kinoti.

Walaghai wamekuwa wakipigia watu simu na kuwadanganya waathiriwa kuwa ni wafanyakazi wa kampuni za simu au benki kabla ya kuwatapeli.

“Watu hao wamekuwa wakipiga simu na kuwahadaa watu kwamba kuna hitilafu katika akaunti zao za benki, Mpesa au Airtel Money. Waathiriwa wanatoa taarifa muhimu ambazo zinawezesha walaghai kuwaibia fedha,” ikaonya idara ya DCI.

Bw Kinoti pia amewataka Wakenya kuepuka kulipia nyumba za kupanga ambazo hawajathibitisha mmiliki wake au ploti.“Watu wasikubali kulipia nyumba za kupanga au ploti ambazo hawajaziona,” akaonya Bw Kinoti.

Alikiri kuwa kusaka wahalifu hao huwa ni vigumu kwani inahitaji uchunguzi wa kina ambao huhitaji siku nyingi kukamilika.

“Hii ni kwa sababu matapeli hao wanatumia laini za simu kwa kutumia majina ya watu wengine. Baada ya kutekeleza uhalifu wanatupa laini.“Vilevile, akaunti za mitandao ya kijamii huzifuta mara baada ya kutekeleza uhalifu hivyo huwa vigumu kuwanasa na kuwafikisha mahakamani,” akasema Bw Kinoti.

Wahalifu hao hutumia vipakatalishi, laini, simu, vyeti vya kuzaliwa vitambulisho vya kitaifa au laini za simu za wizi.Baada ya kupokonya watu vitambulisho vya kitaifa, wahalifu hao huvitumia kusajili laini ambayo baadaye wanaitumia kutapeli watu.

“Mara baada ya kupoteza kipakatalishi, simu, kitambulisho cha kitaifa na stakabadhi nyinginezo za kibinafsi kama vile vyeti vya masomo au kuzaliwa au leseni ya udereva, ripoti katika kituo cha polisi.

“Ni jukumu la polisi kukabiliana na visa vya uhalifu lakini kuna haja kwa wananchi kuchukua tahadhari ili kuzuia uhalifu wa aina hiyo,” akasema Bw Kinoti.

Kulingana na Sheria kuhusu Uhalifu wa Mitandaoni na vifaa vya Kielektroniki iliyoidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018, mtu anapokosa kurejesha fedha anazotumiwa kimakosa kupitia Mpesa, Airtel Money kati ya huduma nyinginezo anastahili kutozwa faini ya Sh200,000 au kifungo cha miaka miwili gerezani.

You can share this post!

DCI yachunguza kisa cha watoto kufungwa

Kubu kuongeza ladha ya Fiji kikosini Shujaa kwenye Raga ya...