HabariSiasa

Ukoloni wa China nchini wanukia

June 13th, 2019 2 min read

BENSON MATHEKA Na KAMAU WANDERI

KENYA imo kwenye hatari ya kuwa chini ya ukoloni wa China ikiwa haitachukua hatua za kuepuka madeni na kuzuia raia kutoka nchi hiyo kuongezeka nchini.

Hatari hii inatokana na kuwa Kenya ikishindwa kulipa madeni hayo, China inaweza kutwaa mali ya Kenya yakiwemo mashamba, bandari, reli na miundomsingi mingine muhimu kitaifa.

Idadi kubwa ya Wachina wanaofanya biashara za mitumba, samaki, mayai na kazi zinazoweza kufanywa na Wakenya pia inatia wasiwasi kuwa wageni hao hatimaye watakuwa na uwezo hata wa kisiasa nchini.

Pia wameanzisha mafunzo ya lugha ya Kichina katika vyuo vya humu nchini.

Kampuni za kimataifa za China pia zimepenya katika mashirika muhimu ya serikali. Katika Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) ni kampuni za China, Pang na StarTimes zinazofanikisha mfumo wa utangazaji wa dijitali nchini.

Shirika la habari la China, Xinhua, nalo linasambaza habari kwa vyombo vya habari hapa Kenya bila malipo.

Hapo jana Serikali ilitetea kuongezeka kwa raia wa China nchini ikiwataja kama baraka kubwa kwa Wakenya.

Kulingana na Waziri wa Mawasiliano, Joe Mucheru, Wakenya wamefaidika pakubwa kutokana na Wachina wanaofanya biashara nchini kwani hawahitajiki kusafiri China kupata baadhi ya bidhaa.

“Sijui tunalalamikia nini. Wafanyabiashara hao wametusaidia sana kwa vile kando na kutuletea bidhaa, wametufaa sana katika masuala ya uvumbuzi wa kiteknolojia,” akasema Bw Mucheru akiwa Chuo Kikuu cha Nairobi.

“Ni kinaya kwamba tunalalamikia faida kubwa ambayo tunapata kutokana na Wachina hao, badala ya kufurahia mchango wanaotoa kwa ukuaji wa uchumi wetu,” akasema.

Lakini Serikali ilionekana kujikanganya kwani Bw Mucheru akitamka hayo, naye Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alikuwa akiagiza kufurushwa kwa Wachina wanaofanya biashara na kazi ndogo ndogo nchini.

Lakini agizo la Dkt Matiang’i halina uzito kwa sababu Wachina hao wako hapa nchini kwa njia halali kwa mujibu wa sheria ya uhamiaji.

China ina mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na Kenya, ambao unaruhusu mashirika na raia wa nchi hiyo kushiriki biashara nchini.

Raia wa nchi hiyo wamekuwa wakitumia mkataba huo kupata vibali vya kufanya kazi na kuuza bidhaa zinazoweza kuuzwa na Wakenya.

Wafanyabiashara Wakenya wanasema hawawezi kushindana na Wachina kwani wanauza bidhaa zao kwa bei ya chini.

Idadi ya wageni hao pia imeongezeka kupitia kwa kampuni za China zinazopatiwa zabuni nchini, kwa sababu huwa zinawaleta raia kutoka nchi yao kufanya kazi hapa badala ya kuwaajiri Wakenya.

Katika mfumo inayotumia kupatia Kenya mikopo, China inahakikisha ni raia wake wanaotekeleza miradi husika na kuisimamia hadi walipwe madeni yao yote.