Habari Mseto

Ukosefu wa chakula walazimisha watoto kugura masomo

February 6th, 2019 1 min read

Na SAMMY LUTTA

WALIMU katika Kaunti ya Turkana wamelalamikia hali ya idadi ya watoto wanaofika shuleni kupungua kwa kiwango kikubwa katika shule za msingi, baada ya mradi wa kuwapa chakula cha bure ulioanzishwa na serikali kuu kusimamishwa.

Baadhi ya walimu wakuu, haswa wanaotoka maeneo yaliyo na umaskini mkubwa walisema kuwa wamelazimika kutumia pesa za mishahara yao kuwanunulia chakula watoto ili wasalie shuleni.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Katapakori Dominic Echoto alisema kuwa watoto wengi wanapotoka nyumbani kwao wanatarajia kulishwa shuleni, na hivyo wanapokosa chakula wanakosa kuhudhuria masomo.

“Sasa kwa kuwa hakuna chakula, idadi ya wanafunzi wanaofika shuleni imerudi chini. Muhula uliopita wakati kulikuwa na chakula, shule yangu ilikuwa na zaidi ya watoto 250 lakini sasa wamesalia takriban 90,” Bw Echoto akaeleza Taifa Leo.

Mwenyekiti wa Muungano wa Walimu (KNUT) tawi la Turkana Kenyaman Aring’oa alisema kuwa umekuwa mtindo kwa watoto kuhudhuria masomo mahali ambapo kuna chakula.

“Shule iliyoko maeneo ya ndani inapokosa chakula inapoteza watoto katika madarasa yote. Kwa hivyo, ninasihi serikali kuu kuharakisha kufikisha chakula katika shule hizi,” akasema Bw Ariong’oa.

Alisema kiwango cha elimu katika kaunti hiyo kinategemea sana namna chakula kinafikishwa shuleni.

Walimu walisema maeneo saba ya Turkana ya Kati, Kaskazini, Kusini, Mashariki, Magharibi, Loima na Kibish yameaThirika na hali hiyo.

Mradi huo wa kutoa chakula kwa shule ulichukuliwa na serikali kuu kutoka kwa mradi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP)mwaka uliopita, baada ya mradi huo kuwepo tangu miaka ya themanini.