Habari Mseto

Ukosefu wa fedha za kutosha watatiza utafiti kuhusu kuharibika kwa mandhari ya maziwa

September 6th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

UTAFITI unaoendelea kuhusu kudorora kwa hali na mandhari ya baadhi ya maziwa hapa nchini unaonyesha kuwa fedha zinazotengwa kwa utafiti huo hazitoshi.

Kulingana na watafiti chini ya shirika la Institute for Climate Change and Adaptation (ICCA), miradi mingi kuhusu maziwa inategemea wafadhili na wala sio serikali.

Watafiti hao walisema kuwa serikali kuu pamoja na zile za kaunti zinatenga kiwango cha chini sana cha fedha, jambo ambalo limesababisha ugumu katika utekelezaji wa mapendekezo.

“Marupurupu yanayotokana na mapato madogo kama vile leseni za uvuvi na utalii hayatoshi kusimamia miradi ya utafiti kuhusu uharibifu wa maziwa,” ilisema ripoti hiyo iliyoandaliwa na Prof Daniel Olago, Jackson Raini na watafiti chini ya International Lake Environment Committee (ILEC).

Kwa sasa watafiti hao wanaangazia maziwa matatu ambayo ni Ziwa Victoria, Ziwa Nakuru na Ziwa Baringo.

“Kufikia sasa hakuna ofisi maalum serikalini ambayo inahusika na maswala ya maziwa na ni jambo la kutia hofu,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Wanasayansi bado hawajaweza kujibu baadhi ya maswali kuhusu kufurika kwa maziwa hasa yale ya Bonde la Ufa.