Habari Mseto

Ukosefu wa hela umeeneza corona kwenye kaunti – Magavana

November 21st, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KUCHELEWESHWA kwa fedha za kaunti na Hazina Kuu kumechangia pakubwa kuongezeka kwa maambukizi ya Covid-19 maeneo ya mashinani.

Magavana wanadai hawana pesa za kuwanunulia vifaa vya kujikinga (PPEs) maafisa wanaotoa huduma za afya.

Ukosefu wa PPEs kumechangia pakubwa kuambukizwa kwa maafisa wa afya na gonjwa hili.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya alisema kaunti zimekosa fedha za kujistawisha kwa vile hazijapata mgawo kutoka hazina kuu ya serikali tangu mwezi Agosti mwaka huu.

Bw Oparanya alisema kaunti zinakabiliwa na change moyo chungu nzima kutokana na ukosefu wa fedha kutoka kwa wizara ya hazina ilhali wananchi wanataka kupata huduma maridhawa.

Bw Oparanya aliitaka bunge la seneti limwagize Waziri wa Hazina Ukur Yatani afike mbele yake kueleza kinacho sababisha kucheleweshwa kwa kutolewa kwa fedha za kaunti.

“Maseneta wanatakiwa kuyazipa maslaha ya kaunti kipau mbele kwa kuhakikisha zimepata mgawo wake kutoka kwa hazina kuu katika muda unaofaa,” alisema Bw Oparanya.

Alisema kaunti zimeshindwa kupambana ipasavyo na kusambaa kwa Covid-19 kwa sababu ya ukosefu wa vifaa.

“Tunawasikitia wahudumua wa afya haswa wanaofanya kazi katika maeneo wanakotengwa walioambukizwa Covid-10 kwa vile hakuna kitu tunaweza kufanya kwa vile wizara ya fedha imekataa kutoa fedha za kununua vifaa na madawa ya kupambana na janga hili,” aliongeza kusema.

Mwenyekiti huyo wa CoG alielezea hofu kwamba serikali haitazipa kaunti nyongeza ya asili mia 35 ya fedha kwa kaunti ikitiliwa maanani imeshindwa kutoa asilimia 15.

Akizugumza katika uwanja wa michezo wa Mumias wakati wa maombi ya mazishi ya aliyekuwa msimamizi wa huduma za wafanyakazi kaunti ya Kakamega Bw Robert Sumbi, Bw Oparanya alisema ni vigumu sasa kwa kaunti kutoa huduma ikitiliwa maanani hazijapata mgawo kutoka hazina kuu za miezi ya Septemba, Oktoba na Novemba.

Alidokeza kuwa magavana kutoka eneo la ziwa Victoria walikutana na wenzao kutoka Kisii mjini Kisumu wiki iliyopita na kuafikiana kuwa wataunga mkono mchakato wa maridhiano wa BBI kwa vile umetoa mapendekezo ya kusuluhisha shida zinazokumba serikali za kaunti.

Bw Oparanya alisema: “Ijapokuwa BBI haiku asili mia moja sawa tunahitaji kuiunga mkono.Upungufu uliopo utarekebishwa wakati wa utekelezaji ndipo mshikamano nchini upatikane.”

Wabunge Benjamin Washiali (Mumias mashariki) na Cleophas Malala (Seneta wa Kakamega) na aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa waliunga kuahirishwa kwa zoezi la kukusanya saini milioni moja kuwezesha mashauriano kufanyika.

Bw Washiali alisema maoni ya kila mmoja yanapasa kushirikishwa katika ripoti BBI.