Habari

Ukosefu wa maji washuhudiwa Thika

February 23rd, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MAENEO mengi mjini Thika yanaendelea kukosa maji safi ya kunywa huku wakazi wakitaka kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd kuingilia kati kutoa suluhisho.

Wakazi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mitaa wanakoishi zinakosa maji huku wakilazimika kutafuta maeneo mengine ama kununua kwa wachuuzi.

Mitaa iliyoathirika kutokana na ukosefu huo ni Landless, Muguga na Kisii mjini Thika.

Bw Joseph Kimani wa mtaa wa Landless, Thika, anasema watu wachache wamechimba maji ya visima lakini anadai maji hayo sio safi ya kunywa kwa sababu yanaonja chumvi.

“Wakazi wengi wa hapa wamekuwa na matatizo ya maji kwa muda mrefu na kwa hivyo tunaiomba kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd waingilie kati kuona ya kwamba wanasambaza maji hadi maeneo haya,” alisema mkazi huyo.

Hata hivyo katika mkutano wa kila mwaka ulofanyika mjini Thika mnamo Ijumaa, mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Thiwasco, Bw Moses Kinya, alisema tayari wanafanya mikakati kuona ya kwamba wananunua mabomba ya kisasa ya kusambaza maji.

“Kumekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji katika mitaa kadhaa Thika na kwa hivyo kampuni ya Thiwasco inafanya juhudi kuona ya kwamba wakazi wa mitaa hiyo wanapata maji baada ya wiki chache zijazo,” alisema Bw Kinya.

Alisema mabomba ya maji yaliyokuwepo hapo awali ni madogo kwa upana na kwa hivyo hayatoshelezi mahitaji ya wateja wao.

Alisema pia kwa wakati huu kampuni hiyo inahudumia wakazi wa Thika na vitongoji vyake; watu wapatao 300,000 baada ya wao kuongezeka.

Alisema kulngana na changamoto hiyo ni sharti watafute njia mwafaka kuona ya kwamba wanatosheleza mahitaji ya wateja wao kwa njia ifaayo.

Alizidi kueleza ya kwamba watazidi kutumia teknolojia ya kisasa kwa usambazaji wa maji hayo ili kutosheleza mahitaji ya wakazi hao.

Mnamo Jumamosi mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema shida ya maji imekuwa changamoto katika maeneo mengi Thika na vitongoji vyake.

“Tayari nimefanya mipango ya kuona ya kwamba siku chache zijazo mtambo wa kuchimba maji unaanza mradi huo katika maeneo yaliyoathirika kwa kukosa maji. Tunalenga maeneo ya Landless, Kilimambogo, na Ngoliba ambapo kazi itaanza mara moja,” alisema Bw Wainaina.

Alisema mabomba ya kusambaza maji katika kituo cha Ngoliba yalipelekwa huko miezi mitatu iliyopita ambapo kile kilichobaki ni kuyaunganisha baada ya uchimbaji wa maji ili bidhaa hiyo iwafikie wananchi.