Ukraine yakomoa Macedonia Kaskazini na kusajili ushindi wa kwanza kwenye Euro

Ukraine yakomoa Macedonia Kaskazini na kusajili ushindi wa kwanza kwenye Euro

Na MASHIRIKA

BAADA ya kupoteza mechi yao ya kwanza kwenye fainali za Euro, Ukraine walijinyanyua mnamo Alhamisi na kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Macedonia Kaskazini katika mechi ya Kundi C iliyochezewa jijini Bucharest.

Ukraine walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo baada ya Uholanzi kuwapokeza kichapo cha 3-2 mnamo Juni 13 katika mechi ya kwanza ya Kundi C.

Chini ya kocha Andriy Shevchenko, ushindi wa Ukraine dhidi ya Macedonia Kaskazini ulisaidia kikosi hicho kukomesha rekodi mbovu ya kupoteza jumla ya michuano sita mfululizo kwenye kampeni za Euro.

Ni ufanisi uliowasaza katika nafasi nzuri ya kusonga mbele na kuingia hatua ya mwondoano kundi Kundi C ambalo pia linajumuisha Austria.

Nahodha Andriy Yarmolenko anayechezea West Ham United katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), alichuma nafuu kutokana na utepetevu wa mabeki wa Macedonia Kaskazini na akafunga bao la kwanza katika dakika ya 29 kabla ya Roman Yaremchuk kufunga bao la pili kunako dakika ya 34.

Fowadi Ezgjan Alioski anayechezea Leeds United aliwarejesha Macedonia Kaskazini mchezoni katika dakika ya 57. Bao alilolifunga lilikuwa zao la penalti iliyopanguliwa na kipa wa Ukraine.

Ingawa goli hilo liliwapa Macedonia Kaskazini motisha zaidi ya kuvamia lango la wapinzani wao, walishindwa kupata bao la kusawazisha licha ya kipa Stole Dimitrievski kupangua penalti ya fowadi Ruslan Malinovskiy wa Ukraine mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ukraine kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Austria katika mchuano wa mwisho wa Kundi C mnamo Juni 21 huku Macedonia Kaskazini wakichuana na Uholanzi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Saa za kafyu zaongezwa kaunti 13 zilizoko Magharibi, Nyanza

‘Maradona alifariki kutokana na utepetevu na mapuuza...