Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Aibu ya mapenzi

October 15th, 2019 1 min read

Na PHYLLIS MWACHILUMO

MAPENZI ni matamu kweli, yana nguvu ya kuivunja milima na kuyeyusha roho ngumu zilizozidi chuma.

Pia husemekana kuwa kama kikohozi, hayafichiki. Sijui kwa vipi hasa ila nadhani huku kutofichika kwake ndiko huweza kuwa chanzo cha aibu kwa kiasi kikubwa sana.

Watu wanapopendana, huwa hawamwogopi yeyote. Utamsikia binti mchanga amekuwa mjeuri kwa wazazi, kisa na maana ni kukatazwa kuonana na mpenziwe.

Vilevile, wazee hujiona kuwa wadogo tena kiumri, kuwa wamezaliwa upya pindi tu wanapopata wapenzi.

Haya ya wazee kupenda huweza kutukumbusha Mzee Mwinyi katika riwaya ya ‘Kiu’ (Mohamed S. Mohamed).

Mzee Mwinyi kwa kweli hakujali lolote ilmradi awe na mpenzi wake Bahati.

Hakujali hasara ya hali na mali bora tu ampate huyo Bahati wake.

Hata hivyo kunao wengi wanaojipata katika mateso wakidai ni mapenzi.

Kisingizio cha mapenzi

Wengi huhadaiwa na kuteswa na ‘wapenzi’ bandia wenye kujaa ubinafsi na kujua wazi kuwa wanatumia kisingizio cha mapenzi.

Aibu ya mapenzi ni kule kutokujali waliokuzunguka, dunia nzima huishia kuwa ya hao wapenzi wawili tu.

Kwa wakati huo, huwa hawasikii la nani wala nani. Ama kweli kipendacho roho…

Kwa ufupi, mapenzi hulemaza, yakawaacha walevi wake wakiwa hoi katika upofu wa ajabu wasiweze kuona mbele wala nyuma.

Ila, pindi tu upofu huu unapoisha, yote huwa wazi na mwangaza wa ukweli sasa huwaangazia wakaona vyema yote yaliyokuwa yamefichika.