Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Aina za lugha

April 5th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

LUGHA mwiko

Hii ni aina ya lugha ambayo matumizi yake yamefungiwa katika vigezo fulani vya utamaduni. Lugha mwiko pia inasheheni msamiati mahsusi ambao hauruhusiwi kutumiwa kiholela katika jamii. Mifano ni kama vile:

 1.             sehemu nyeti za mwili
 2.             msamiati wa ngono na kadhalika.

Msamiati huu huhusisha maneno ambayo hutamkwa katika mazingira fulani maalumu pekee. Madhumuni ya lugha mwiko katika jamii ni pamoja na:

 1. Kukuza uhusiano mwema katika jamii.
 2. Kuhifadhi maadili na imani za jamii.
 3. Kuhifadhi na kuhami mambo muhimu ya jamii yasiathirike na mambo ya kigeni

Lingua franka (Lingua franca)

Lugha hii hutumiwa na watu walio na lugha tofauti kwa ajili ya mawasiliano. Mfano mzuri ni Kiswahili ambayo ni lingua franka katika eneo la Afrika Mashariki.

Sifa za Lingua Franka ni kama zifuatazo:

 1. Hukiuka mipaka ya kitamaduni.
 2.  Hukutanisha watu wa asili mbalimbali.
 3. Hukiuka mipaka ya kimaeneo kwa kuwa hutumika katika eneo pana zaidi.
 4. Hutumiwa na watu ambao lugha mame zao ni tofauti.
 5. Ni lugha ya mawasiliano kati ya watu wenye lugha zaidi ya moja.
 6. Yaweza  kuwa lugha ya kwanza au ya pili ya mzungumzaji na kwa wengine lugha ya kigeni.

 Lugha za taifa

Hizi ni lugha za asili za kikabila zinazozungumzwa katika nchi fulani mathalan baadhi ya lugha zinazozungumzwa nchini Kenya ni kama vile: Kikikuyu, Kiluhya, Kikamba nchini Kenya.

Nchini Tanzania kuna lugha kama vile: Kihaya, Kisukuma, Kibondei.

Pijini (Pidgin)

Hii ni lugha inayobuniwa na kutumiwa kwa mawasiliano baina ya watu ambao lugha zao ni tofauti na hawana lugha moja wanayoielewa kwa pamoja.

Sifa za pijini ni kama zifuatazo:

 1. Haina wazungumzaji wazawa.
 2. Huzuka baina ya lugha tofauti kabisa kitamaduni.
 3. Huwa na miundo hafifu ya kisarufi.
 4. Ina msamiati finyu sana.
 5. Huwa lugha ya hadhi ya chini inayopigwa vita ili ife.
 6. Msamiati mwingi wa pijini hutegemea sana mojawapo katika lugha zinazo wakutanisha watu.
 7. Huwa na fonimu chache.
 8. Hutumia ishara kwa wingi kwa sababu ya uhaba wa msamiati.

 

[email protected]

Marejeo

Chiraghdin, S., Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, J.C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers.