Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Alama ya kistari kifupi, ritifaa na nuktakatishi katika uakifishaji

May 8th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

TUMEKUWA tukichambua na kujifahamisha kuhusu alama mbalimbali za uakifishaji na matumizi yake sahihi katika uandishi.

Hii leo tutajadili na kupambanua kwa kina kuhusu alama zifuatazo katika uakifishaji.

Matumizi ya Kistari kifupi, Kistariungio, Kiungo (-)

Katika makala ya leo, tutaangazia alama ya kituo cha kistari kifupi au ukipenda kistari ungio au kingo katika uakifishaji.

Sawa na jina lake linavyoashiria, alama ya kistari kifupi ni tofauti na kituo cha kistari kirefu almaarufu deshi ambapo matumizi yake yanatofautiana vilevile.

Kituo cha kistari kifupi hutumika kwa usahihi kwa njia ifuatayo:

Alama ya kiungio hutumika wakati wa kukata neno hasa kwenye ukingo wa karatasi wakati nafasi ya kuandika neno zima inapokosa.

Inapotumika kwa namna hiyo, alama ya kistari kifupi huashiria kuwa neno ambalo halijakamilika litaendelezwa katika msitari ufuatao. Kwa mfano:

Virusi vya corona vina-

zidi kusambaa nchini.

Wanafunzi wanatazamiwa ku-

rejea shule mwezi Juni.

Unapotumia kituo neno kwenye silabi badala ya kwenye konsonanti. Kwa mfano:

wana – (sahihi)

funzi

wan-

afunzi (haifai)

Kituo cha kistari kifupi pia hutumika kuonyesha umbali, kipindi, muda au wakati baina ya nyakati mbili.

Aghalabu, katika mazingira haya, kituo cha kistari kifupi hutumika badala ya maneno ‘mpaka’ au ‘hadi.’

Mazoezi ya ziada ni kutoka ukurasa 20-25

Uchumi uliimarika pakubwa miaka ya 2010-2015

Tutasaoma kitabu cha Mhubiri 3:1-7

Isitoshe, alama ya kistari kifupi hutumika wakati wa kupanga au kuorodhesha vipengele au mawazo makuu kwa mukhtasari.

Katika mazingira haya, alama ya kiunguo huwekwa mwanzoni mwa kila sentensi. Kwa mfano:

Mwaka huu wa 2020 kumekuwa na majanga kama yafuatayo:

Nzige wa jangwani

Mafuriko

Maporomoko

Mkurupuko wa Covid-19

Alama ya kistari kifupi pia hutumiwa kuunganisha maneno mawili ili kuunda jina moja. Kwa mfano:

Paka-shume

Mbwa-mwitu

Mbwa-koko

Mwana-haramu

Pilipili-manga

Kitunguu-saumu

Mwana-kondoo

Madongo-poromoka

Aidha, kituo cha kistari kifupi hutumika kama alama ya hisabati ya kutoa au kupunguza.

30-20 = 10

100-99 = 1

[email protected]

Marejeo

Leech, G. (1983). Principles of Pragmatics. London: Longman.

Makombo, H. & Wachira, W. (2008). Misingi ya Kiswahili 4 (MWF), Dar es Salaam: Ujuzi Books Ltd.

Masood, A. J. (2013). Kiswahili kwa Shule za Msingi 3 (MWL), Dar es Salaam: Educational Books Publishers Ltd.