Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Alama za uakifishaji ambazo kila mwandishi anapaswa kuzifahamu

March 28th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

TUMEKUWA tukitathmini kuhusu uandishi wa kiubunifu.

Katika makala ya leo tutaangazia kuhusu dhana na dhima ya uakifisahaji ikiwemo alama anuwai zinazotumika katika uakifishaji.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Oxford, dhana au ukipenda maana ya uakifishaji ni uwekaji wa alama za uandishi kama vile nukta, koloni na kadhalika.

Aidha, inaweza kuelezwa kama matumizi ya alama mbalimbali katika fungu la maneno ili kuweza kuelewa maana.

Dhima kuu ya uakifishaji ni kuwezesha msomaji kuyasoma yale yameandikwa kwa urahisi na kuyaelewa vilivyo.

Iwapo mwandishi hataafikisha vyema kazi yake ya uandishi, basi anakabiliwa na tishio la kupoteza maana aliyokusudia kuwasilisha kwa hadhira lengwa pamoja na kumkanganya msomaji.

Hivyo basi, ni sharti kila mwandishi ajifahamishe vyema na ajitahidi kutumia ipasavyo alama mbalimbali za uakifishaji.

Kuna alama mbalimbali za uakifishaji ambazo zinaweza kuainishwa katika vitengo sita tofauti kuambatana na dhima au ukipenda kazi yake kama ifuatavyo.

Alama za uakifishaji zinazotumika katikati au ndani ya sentensi.

Alama za uakifishaji zinazotumika katika mwisho wa sentensi

Alama za uakifishaji za kuunganisha vitu mbalimbali katika sentensi

Alama zinazotumika kutenganisha maneno au virai vivumishi ambavyo hutoa habari zaidi juu ya sentensi.

Alama za uakifishaji zinazotumika kufungia au kusisitiza maneno au vifungu vya maneno vinavyoingilia au kukatiza muundo wa sentensi.

Alama za uakifishaji wa kutenganisha maneno au virai vilivyodondolewa na sehemu nyingine ya sentensi.

Alama zinazotumika katika mwanzo wa sentensi au majina maalum

Herufi kubwa

Katika uandishi, herufi kubwa hutumiwa katika mazingira yafuatayo:

Kila unapoanza sentensi, herufi ya kwanza ya neno la kwanza katika sentensi inapaswa kuwa kuanza kwa herufi kubwa.

Neno hili laweza kuwa la kwanza katika sentensi ya kwanza ya habari au aya au neon maalum

Tumia herufi kubwa pia baada ya alama za uakifishaji zifuatazo: nukta, kiulizo, mshangao, alama za nukuu na nukta pacha.

Wakati wa kuandika herufi ya kwanza ya majina yafuatayo:

Majina ya watu, nchi, mji, nchi, bara, na kadhalika kwa mfano, majina ya pande za dira: Kaskazini, Kusini, Mashariki, Magharibi, Kaskazini Mashariki, Kusini Magharibi na kadhalika.

 

Wasiliana na mwandishi kwa kutumia baruapepe: [email protected]

Marejeo

Leech, G. (1983). Principles of Pragmatics. London: Longman.

Makombo, H. & Wachira, W. (2008). Misingi ya Kiswahili 4 (MWF). Dar es Salaam: Ujuzi Books Ltd.

Masood, A.J. (2013). Kiswahili Kwa Shule za Msingi 3 (MWL). Dar es Salaam: Educational Books Publishers Ltd.