Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Athari za lugha ya kigeni kwa walimu, wanafunzi katika kuendeleza elimu

March 23rd, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KWA mujibu wa watafiti kama vile Senkoro, uwezo wa kung’amua na kueleza mtazamo na hisia za ndani kuhusu maarifa ndiyo msingi wa ubunifu na ugunduzi.

Matumizi ya lugha ya kigeni, husababisha hata walimu kukosa uwezo unaostahili wa kufundisha na wanafunzi kushindwa kuelewa kile wanachojifunza.

Mwinsheikhe (2003) katika utafiti wake uliolenga kujua kama kutumia Kiswahili katika mchakato wa kufundisha na kujifunza kunaweza kuimarisha ushiriki na ufaulu wa wanafunzi kwa masomo ya sayansi. Aligundua kwamba, kuna tatizo la lugha katika kufundisha somo la sayansi.

Walimu wengi walikiri kutumia lugha ya Kiswahili wanapofundisha masomo hayo kinyume na sera ya elimu ya Sekondari. Aidha, wanafunzi walisema kwamba, wao wanatumia Kiswahili zaidi katika mijadala ya masomo yote ya sayansi.

Lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia katikashule ya upili imezidi kukumbana na vikwazo chungunzima ambavyo vimechangia katika kushindwa kuelewa masomo kwa umakini darasani.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na HakiElimu (2007) ulibaini kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi wa sekondari hawajui lugha ya Kiingereza kwa ufasaha na walishindwa ama kusoma au kutafsiri aya rahisi ya Kiingereza iliyoandaliwa kwa ngazi ya darasa la pili.

Aidha, utafiti huo unafafanua kwamba huwezi kutarajia mwanafunzi asiyejua Kiingereza kuelewa masomo darasani na hatimaye kufaulu mtihani.

Kwa mujibu wa Missokia na Zombwe (2007) kushuka kwa matokeo kwenye mitihani ya kidato cha nne 2010 kulichangiwa na wanafunzi wa shule za kata kutojua lugha ya kufundishia elimu ya Sekondari.

Watafiti hao walibaini kuwa walimu wa Sekondari wanapata shida sana kufundisha kwa lugha ya Kiingereza.

Walieleza kwamba, lugha ya kufundishia ni muhimu sana kwa wanafunzi na walimu kuweza kuielewa kikamilifu ili kuwawezesha kuwasiliana na kujifunza.

Lugha pia inaweza kuwa kikwazo kikubwa katika kuchangia kushuka kwa kiwango cha elimu iwapo wanafunzi hawaimudu. Hii kwa sababu watashindwa kupokea maarifa kikamilifu hivyo kushindwa kujieleza ipasavyo.

Kwa mantiki hiyo ni wazi kuwa lugha ya kufundishia ina athari kubwa kwa mstakabali wa elimu ya kiwango husika.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Bryman A. (2008). Social Research Methods. London: Oxford University Press.

Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two solitudes assumption in Bilingual education.In J. Cummins & N.H Homberger (Eds),Encyclopedia of Language and Education,2nd Edition,Volume 5.New York:Supringer Science + Business Media LLC.

Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University.