Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Athari zinazowakabili walimu kwa kutumia lugha ya kigeni katika kufundishia

March 23rd, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

INASIKITISHA kwamba licha ya wataalamu kugundua kuwa lugha ya kufundishia ina athari hasi bado hawajavumbua mbinu za kusuluhisha matatizo hayo.

Isitoshe, wataalamu wameshindwa kufafanua ni nini kinachosababisha walimu wa sekondari kutojua vyema lugha ya kufundishia.

Kueleza tafiti zinazohusiana na ukuaji wa lugha, madhara ya matumizi ya lugha za kigeni katika kufundishia elimu kwa ujumla na tafiti kuhusu ni kwa nini watunga sera hawakipi kipaumbele Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia elimu.

Aidha, jinsi tafiti zinavyoonyesha, Kiswahili kimekua sana, na kina hadhi kubwa katika ukanda wa Afrika mashariki na kati, na sehemu nyinginezo.

Pamoja na ukuaji huo wa lugha ya Kiswahili, hakuna tafiti za siku za karibuni zilizofanywa kuhusiana na haja ya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia elimu.

Rubagumya (1990) anatoa hoja kwamba ni muhimu kujua ni lini Kiswahili kitakuwa lugha rasmi ya kufundishia kiwango cha shule ya sekondari.

Tunaelewa kwamba lengo kuu la kutangaza Kiswahili kama lugha rasmi ya kufundishia elimu ya msingi mwaka 1967 nchini Tanzania, lilikuwa ni kukifanya kiwe lugha ya kufundishia elimu ya sekondari ifikapo mwaka 1974.

Kukosa mawasiliano

Changamoto zinazowakabili walimu ni kukosa mawasiliano mazuri darasani, kiasi kinachofanya washindwe kuelewana na wanafunzi hatimaye wanafunzi kushindwa kupata maarifa yaliyokusudiwa kwa kiwango hicho.

Alidou na Brock-Utne (2005) wanadai kwamba ujuzi mdogo wa lugha ya kufundishia una athari hasi kwa ufundishaji.

Vinke na wenzake (1998) walibaini kwamba, nchini Uholanzi walimu wanakabiliwa na changamoto ya kimawasiliano.

Walimu hawana ujuzi wa kutosha kutumia lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya kufundishia.

Vinke na wenzake wanaeleza kwamba walimu wana uzito wa kutamka na hawana uwezo wa kujieleza kwa kutumia lugha ya Kiingereza wakati wa kufundisha na baada ya vipindi hutumia lugha ya wenyeji zaidi.

Wilkinson (2005) anadai kwamba nchini Uholazi walimu wanashindwa kutumia lugha ya kufundishia kwa mawasiliano mazuri.

Aghalabu hubadili msimbo kutoka lugha ya kufundishia ambayo ni Kiingereza kwenda lugha ya wenyeji ili wanachofundisha kiweze kueleweka vyema.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Rugemalira, J. M. (2005). Theoretical and Practical Challenges in a Tanzanian English Medium School. Africa and Asia

Senkoro, F. (2004). The role of language in education and poverty alleviation: Tool for access and empowerment in Justian Galabawa and Anders Narman Education poverty and Inequality (eds.Dar es Salaam.KAD Associates

Skutnabb-Kangas, T. & McCarty, T. L. (2008). Key concepts in bilingual education: Ideological, historical, epistemological and empirical foundations. In J. Cummins and N. H. Hornberger (Eds.), Encyclopedia of Language and Education, 2nd Edition, Volume 5: Bilingual Education. New York: Springer Science + Business Media LLC