Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Chimbuko la Nadharia ya Utambulisho

June 26th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MWASISI wa Nadharia ya Utambulisho ni msomi Howard Giles (1982).

Nadharia hii imeendelezwa kutoka kwa Nadharia ya Mawasiliano ya Usemi (Speech Communication Theory) ya Leech (1976).

Kwa mujibu wa Giles na wenzake (2005), Nadharia ya Mawasiliano ya Usemi ilinuia kueleza hali zinazosababisha mabadiliko katika usemaji kwenye maingiliano ya watu na matokeo ya ubadilishaji huo.

Nadharia hii imepanuka kwani haishughulikii namna ya unenaji pekee, bali pia maingiliano mengine ambayo si ya unenaji kama ishara na maandishi.

Mawazo makuu ya nadharia hii yanaweza kusawiriwa kwa njia zifuatazo: Watu wanapoingiliana wanabadilishana usemi, sauti, na hata ishara ili kujihusisha na wengine.

Nadharia hii pia huhusika na mahusiano kati ya lugha, muktadha na utambulisho.

Kuna aina mbili za Ujihusishaji. Ujihusishaji wa Makutano na Ujihusishaji wa mwachano Convergence & Divergence).

Kulingana na Wardhaugh (2010), nadharia ya Utambulisho ya makutano na mwachano iliasisiwa na Giles mwaka wa (1982).

Makutano ni namna ambavyo watu hubadili usemi, ishara, na sauti ili kujumuisha washiriki katika mawasiliano.

Jinsi wanavyohoji Giles na Smith (1975).

Watu hawa hufanya hivi ili kupunguza tofauti baina yao na kudhihirisha ujihusishaji wao.

Aidha, watu wanaweza kuwa na makutano kupitia njia mbalimbali mathalani: matumizi ya lugha, matamshi, sauti, tabia zisizo za usemi na kadhalika.

Ni muhimu kukumbuka kwamba sio lazima wajihusishe katika mambo haya yote kwa wakati moja. Hata hivyo, watu wanaweza kuwa na makutano katika kiwango kimoja na kuwa na mwachano katika viwango vingine, jinsi wanavyobaini Giles na Coupland (1991).

Mtu binafsi anaweza kujitolea kujinyima kitu fulani ili naye afaidike kwa kupata ujihusishaji kati yake na wale anaowasiliana nao.

Kwa upande wao Turner na Richard (2010), kuna mambo kadha ambayo yanaweza kusababisha kuleta makutano na ni kama yafuatayo:

i. utamaduni unaofanana

ii. matumizi ya lugha yanayooana

iii. maingiliano tarajiwa,

iv. hadhi,

v. historia

vi. kaida

vii. mamlaka

viii. matamanio ya kibinafsi

Naye John Weiner, (1998) aliyenukuliwa na Wardhaugh anatumia nadharia ya Utambulisho kuelezea namna mbali mbali za uteuzi wa lugha.

 

marya.wangari@gmail .com

Marejeo

Ogechi, N.O. (2002). Mbinu za Mawasiliano Kwa Kiswahili. Eldoret: Moi University Press.

Pride, J.B. (1971 ). The social meaning of Language. London: Oxford University Press.

TUKI (2000). Swahili – English Dictionary . Dar es Salaam : Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili sasa ikiitwa TATAKI.