UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana na dhima ya malipo na ada mbalimbali katika jamii

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana na dhima ya malipo na ada mbalimbali katika jamii

Na MARY WANGARI

WANAJAMII huhitaji bidhaa na huduma mbalimbali ili kuwawezesha kufanikisha mambo, kukidhi haja na kuendeleza shughuli za maisha ya kila siku.

Ili kupata bidhaa na huduma mbalimbali aghalabu mtu hutakiwa kulipia malipo au ukipenda ada fulani.

Katika makala ya leo, tutaangazia kwa kina na kufafanua kuhusu dhana ya malipo almaarufu ada, aina mbalimbali za malipo na jinsi yanavyotumika katika maisha ya kila siku katika jamii.

Dhana na dhima ya malipo au ada – Kwa mujibu wa kamusi huru, malipo ni hela au kitu anachotoa binadamu ili kupata bidhaa aliyonunua au huduma aliyopokea.

Kando, na ununuzi wa bidhaa na huduma, malipo yanaweza pia kutumika kama tuzo au zawadi kuashiria shukrani kwa jambo nzuri alilofanyiwa mtu.

Aidha, malipo yanaweza kutumika kama namna ya kuomba radhi, kutuliza hasira au kumrai mtu aliyekwazwa.

Aina ya Malipo – Kuna aina mbalimbali ya ada zinazotumika katika jamii.

Kama mwanafunzi au mwalimu wa lugha ya Kiswahili, ni muhimu kuzifahamu ada hizo mbalimbali na dhima yake ili kuzitumia kwa ufasaha na njia sahihi.

Ifuatayo ni orodha ya ada mbalimbali ambazo huenda umewahi kuzilipa au utakumbana nazo katika katika shughuli za kila siku katika jamii.

Nauli – hii ni ada inayolipwa kwa huduma za kusafiria kama vile matatu, basi, treni, ndege, na kadhalika.

Kivusho – Hii ni ada inayolipwa ili kuvuka mto, daraja, feri au kivuko chochote.

Masurufu – Hizi ni pesa anazopatiwa mtu kugharamia matumizi ya nyumbani au za kutumia anapokuwa safarini.

Koto au ufito – Hii ni ada anayolipa mzazi kwa mwalimu ili kumwingiza au kumsajili mtoto wake shuleni

Karo – Hii ni ada inayolipwa na mwanafunzi ili kupata huduma za masomo shuleni au katika taasisi za elimu.

Kibarua – Haya ni malipo anayopatiwa mfanyakazi baada ya kufanya kazi kwa siku.

Ujira – Ni malipo anayopatiwa mwajiriwa kwa kazi anayofanya katika muda wa chini ya mwezi mmoja. Inaweza kuwa baada ya juma, majuma mawili na kadhalika.

Mshahara – Haya ni malipo anayolipwa mwajuiriwa kila mwezi kwa huduma au kazi anayofanya.

Marupurupu – Haya ni malipo anayopatiwa mwajiriwa ambayo ni zaidi ya mshahara au ujira wake wa kawaida.

Ajari, karisaji au ovataimu – Ni malipo anayopatiwa mwajiriwa kwa muda wa ziada anaofanya kazi.

Kodi ya mapato – Hii ni ada inayolipwa serikali kutokana na mapato ya raia.

Kiinua mgongo au pensheni – Hii ni ada anayopatiwa mwajiriwa baada ya kustaafu kutoka ajira.

Ushuru wa forodha: Hii ni ada inayolipwa kwa serikali ili kuuza au kuingiza bidhaa nchini.

Arbuni, chambele, kishanzu au advansi – Hiki ni kijisehemu cha kwanza cha ada inayolipwa ili kununulia bidhaa na hutumika ili kuzuia isinunuliwe na mteja mwingine. Inaweza pia kuwa kijisehemu cha mshahara anaolipwa mwajiriwa kabla ya malipo yote mwisho wa mwezi.

Riba: Hii ni ada ya ziada anayolipa mkopaji kwa mdeni wake kuhusu mkopo aliochukua. Ni faida inayopata taasisi ya kifedha kama vile benki au mtu binafsi kwa kukopesha pesa.

Karadha – Huu ni mkopo ambao hautozwi riba.

Mtaji – Hizi ni pesa za kwanza anazohitaji mwekezaji au mfanyabiashara ili kuanzisha biashara yake.

Risimu – Hii ni bei ya kwanza inayotajwa katika ununuzi wa bidhaa kwenye mnada.

Fidia – Hii ni ada anayolipwa mhasiriwa kwa hasara au maumivu aliyopata kutokana na kitendo au tukio fulani ambalo lilisababishwa na mtu au kitu kingine.

Faini – Hizi ni pesa anazolipa mshtakiwa kama adhabu kwa hatia aliyopatikana nayo.

Dhamana – Hizi ni pesa anazotoa mshtakiwa ili kumwezesha kuachiliwa huru kutoka kizuizini cha polisi huku uamuzi wa mahakama kuhusu kesi yake ukisubiriwa.

Huweza kuwa pesa taslimu au kupitia bidhaa kama vile mifugo, mvinyo na kadhalika.

Ridhaa – Hii ni ada anayolipwa mhasiriwa kwa kuharibiwa jina au sifa.

Mapoza: Hii ni ada anayolipwa mtu aliyekwazwa ili kumwomba radhi na kutuliza hasira.

Kiingilio – Hii ni ada inayolipwa ili kuingia katika uwanja wa michezo ya spoti, ukumbi wa filamu au michezo ya kuigiza na hafla nyinginezo za burudani.

Mahari – Hii ni ada inayolipiwa mume au mke katika ndoa kutegemea na utamaduni na itikadi za jamii husika.

Tuzo, zawadi, hidaya au takrima – Ni kitu anachotunikiwa mtu kuashiria upendo, nia njema au kumpongeza mpokezi kwa ushindi au kutia fora katika jambo fulani.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

You can share this post!

Hatuna mpango wa kuuza Origi – Liverpool

Jinsi Nakuru ilivyoukaribisha Mwaka Mpya 2021