Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Fafanuzi na nadharia za fasihi

September 3rd, 2019 3 min read

Na ALEX NGURE

WANANADHARIA wengi wamelielezea neno hili fasihi.

Kwa hakika fafanuzi na nadharia juu yake ni nyingi.

Neno fasihi kama linavyoelezewa na wananadharia wote,laonyesha kiwango fulani cha makubaliano kwao kwamba fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia matendo na lugha inayotamkika na kuandikika ili kufikisha ujumbe wake kwa jamii iliyokusudiwa.Zifuatazo ni baadhi ya sifa za fasihi:

Fasihi ni sanaa:

Maana yake ni kuwa fasihi ni matokeo ya kiufundi.Kitu chochote kilichoundwa kwa ufundi hupendeza: huvutia na kuamsha hisia ndani ya mhusika.Hisia hizo zaweza kuwa michomo mbalimbali ambayo yaweza kutufanya tuchukie,tulie, tuhuzunike, tufurahi,tushangae n.k.Ili kazi yoyote ihitimu kupewa jina fasihi,kazi hiyo hudai iwe na uzuri wenye mvuto wa kisanaa-yaani ipendeze; ivutie au iguse hisia za wasomaji au wale wanaolengwa nayo.

Labda kila msanii anapokuwa anabuni kazi yake, anastahiki kuwa na lengo hili.Huu ni mwelekeo wa kutaja kwa ufupi tu sanaa ni nini;kijelezi cha nini sanaa kinaweza kuwanda mno katika marefu na mapana yake.

Fasihi ni matumizi ya lugha kisanaa:

Wataalamu wanaposema kuwa fasihi ni matumizi ya lugha kisanaa,wanamaanisha kuwa fasihi haihusiani na kuwasilisha mawazo tu,bali kuyawasilisha mawazo hayo kisanaa.Haja ya mawasiliano yanayoambatana na sanaa huhitaji kuwasiliana kwa mbinu za kimvuto; ile njia inayompa raha au ladha tamu msomaji anapojaribu kuwasiliana na mwandishi wa kazi ya sanaa.

Fasihi ni kielelezo:

Kauli hii inazingatia ukweli kwamba fasihi haitokei katika ombwe;fasihi haina budi ieleze hali halisi ya maisha ya jamii inayohusika.Kueleza huku hutumia na huzingatia ufundi wa kutumia lugha.Vilevile hubeba ujumbe maalumu ambao unapelekwa kwa jamii inayohusika.Jamii hii huwakilishwa na watazamaji,wasomaji na wasikilizaji.Hawa kifasihi huitwa hadhira.

Fasihi ni maelezo yenye fani na maudhui:

Fani inaundwa na vipengele vifutavyo:matumizi ya lugha, mtindo, muundo, wahusika, mandhari, jina la kitabu n.k.Maudhui nayo huundwa na dhamira, ujumbe, falsafa,migogoro,msimamo wa mwandishi n.k.Kwa maneno mengine, ubora wa kazi ya fasihi hutegemea msanii anavyojali kuoanisha fani na maudhui.

Kwa ufupi, fasihi ni kielelezo cha kisanaa kitumiacho lugha(maneno) kufikisha ujumbe kwa jamii(hadhira) iliyokusudiwa.Vielelezo vya aina hii ni kama vile hadithi,methali,vitendawili,nyimbo,tamthilia,mashairi n.k.Vyote hivi hutumia lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa hadhira fulani iliyokusudiwa.

Tunaposema fasihi ni sanaa; sanaa hapa ni ufundi unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa;umbo ambalo mtu hulitumia katika kutolea hisia zake. Ufundi huo huonyeshwa kwa kutumia sura mbalimbali kama vile maandishi, michoro, ufinyanzi, ususi, uchongaji, ufumaji na kadhalika.

Kazi ya sanaa inatazamiwa ionyeshe ufundi fulani wenye mvuto maalumu kwa hadhira yake.

Matumizi ya picha ni kitu muhimu sana katika utungaji wowote ule.Picha husaidia kuvuta taswira ya kitu kiongelewacho na kikakamata katika akili kwa namna ya ajabu.Hakuna kitu kilicho na nguvu ya maono katika usemaji na utungaji kama picha.Aidha, picha vilevile husaidia sana kuvuta hisi na kuleta mguso wa hali ya juu kwa upande wa mwenye kufikiwa na ujumbe.

Dhima ya fasihi

Kimsingi, fasihi ina dhima nne kuu:

i) Kuelimisha jamii:

-Katika kuelimisha jamii,fasihi huikosoa,huionya na kuirekebisha jamii na inapobidi,hukemea na kulaani matendo yasiyokubalika katika jamii.

-Fasihi ni kioo ambacho kwacho jamii hujitazama na kujitathimini:fasihi huchochea umma na kuwafumbua macho wanajamii ili mathalani,waweze kuuona uozo ulioko katika jamii.

-Fasihi hupiga vita mazingira yote ya ujinga,maradhi,njaa na umaskini katika jamii.

-Fasihi huchochea ari na hamasa na kumfanya mtu asikate tamaa anapopambana na changamoto mbalimbali zinazotokea katika jamii yake.

-Fasihi hueneza mawazo na falsafa ya jamii kwa kupitia tanzu zake kama vile nyimbo, ushairi, hadithi n.k.

-Fasihi hutoa mwongozo jinsi ya kuikomboa jamii kutoka katika fikra mbovu, uonevu wa kitabaka n.k.

ii) Kuburudisha jamii:Kazi mbalimbali za fasihi huburudisha,husisimua kimwili, kiakili na kihisia.

iii) Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii: Fasihi hutunza na kuhifadhi mila na desturi za jamii na pia huweza kurithisha mila hizo kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.

iv) Kudumisha na kuendeleza lugha: Kadiri lugha inavyotumiwa na kufinyangwa na watunzi, ndivyo inavyokua na kupevuka. Maneno mengi yatumiwayo leo katika lugha mbalimbali yalibuniwa awali na kuenezwa na watunzi wa mashairi, riwaya, nyimbo, tamthilia, sanaa za maonyesho na kadhalika.

[email protected]