Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Haja ya Fasihi ya Watoto kukuzwa zaidi kiuandishi na kiuchambuzi

May 14th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

FASIHI ni sanaa inayojihusisha na maisha ya jamaa na jamii.

Ni kioo na mwonzi wa taratibu za maisha ya binadamu na jamii.

Ni sehemu ya utamaduni wa jamii ambayo hujihusisha na maisha ya jamii, na huchota taarifa zake katika jamii na kazi zake hubaki kuwa mali na amali ya jamii. Fasihi huwa ni hazina ya kazi za sanaa.

Hii ina maana kwamba hadithi, mashairi, tamthilia na riwaya huweko kutokana na fasihi simulizi na andishi. Umri wa fasihi ya watoto huwa suala la mjadala kwa kuwa wataalamu hukosa kukubaliana ikiwa fasihi simulizi iliyowalenga watoto inafaa kujumuishwa katika utanzu huu au la.

Wapo wanaoshikilia kwamba ni utanzu mkongwe mno huku wengine wakiamini kuwa ni utanzu mchanga. Fasihi ya watoto ni mpya lakini si mpya kwa maana ya watoto kutohusishwa katika fasihi kwa jumla, bali ni kutokana na kutotazamwa kwa kundi hili kwa upekee katika utanzu na uchambuzi wa kazi ya fasihi.

Pia, fasihi ya watoto ni mpya ikilinganishwa na ile ya watu wazima kwa sababu historia yake si ndefu kwa kuwa imeanza katika Karne ya 18.

Watoto walianza kuchukuliwa kuwa kundi muhimu linalohitaji kutazamwa kwa upekee katika miaka ya 1980 barani Afrika (Traore, 2010).

Ngugi (2011) anakiri kwamba fasihi ya watoto nchini Kenya imekua na kushamiri katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa Bakize (2014) nchini Tanzania, fasihi ya watoto imeshamiri katika miaka ya 1990.

Mashirika mbalimbali yamesaidia kukua na kushamiri kwa fasihi ya watoto kwa kuinua uandishi kama vile ‘British Council’ na ‘Aga Khan Foundation’. Baadaye, mashirika mengine yameongeza nguvu. Nayo ni ‘Book Aid International’ na ‘Pestallozi Children’s Foundation’ (PCF).

Mashirika haya yamesaidia kukua kwa fasihi ya watoto kupitia kwa mradi uliozinduliwa mwaka wa 1991. Mradi mwingine uliosaidia kukua kwa fasihi ya watoto ni ule wa ‘Tusome Vitabu’ uliofadhiliwa na ‘Care International’ kwa kusaidia baadhi ya shule kufungua maktaba za vitabu vya watoto.

Maelezo haya yanaweka bayana kwamba bado fasihi ya watoto ni changa na inahitajika kukuzwa kiuandishi na kiuchambuzi. Ingawa upo mjadala kuhusu maana ya fasihi ya watoto, kuna makubaliano miongoni mwa wataalamu kuhusiana na wanaolengwa na kazi hii.

Utata upo kutokana na umri wa kutumiwa kutenga miaka ya watoto na ya watu wazima. Hili linapozingatiwa, wengi husema ni kazi ambayo kidhamira na kimaudhui huwarejerea watoto au ile iliyoandikwa au kusimuliwa na watoto wenyewe (Nodelman & Reimer, 2003; Wamitila, 2008; Bakize, 2014).

Kwa kujikita katika kigezo cha umri, fasihi ya watoto ni ile inayowahusu watu walio chini ya umri wa miaka 18. Dhana hii ni kulingana na mamlaka ya serikali, mashirika ya kitaifa na kimataifa hususan Shirika la Kazi Duniani (ILO) linalomtambua mtoto kuwa mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18.

Fasihi ya watoto huwa na sifa kadhaa ambazo huitambulisha. Kulingana na Wamitila (2008), sifa hizi ni pamoja kuwepo kwa michoro mingi mizuri ya rangi za kuvutia, lugha rahisi inayoeleweka kwa watoto, iliyosheheni fantasia, mara nyingi huwa na wahusika watoto (kama wahusika wakuu), na hukitwa katika motifu ya safari na msako.

Vilevile huwa na muundo sahili, si ndefu kupindukia na zinajali saikolojia ya watoto. Haya hujitokeza kwa sababu ya umri wa hadhira inayolengwa. Kwa sababu hii ya umri wa hadhira yenyewe, Wamitila (2008) anasema kuwa fasihi hii huathiriwa kwa kiasi kikubwa na mtazamo au mawazo ya jamii kuwahusu watoto.

Itikadi hii inaathiri jinsi tunavyoteua kazi zenyewe za fasihi pamoja na matarajio tuliyonayo kuhusu kazi hiyo; kuandikwa kwayo, dhamira yake, wahusika wake na mwelekeo wake. Fasihi hii inajumuisha nyimbo, mashairi, methali, vitendawili, ngano, hadithi fupi na riwaya.

Uzuri wa kazi za fasihi ya watoto hupimwa kwa kumzingatia mtoto mwenyewe. Vitabu vizuri vya watoto ni vile vinavyowafanya watoto wahisi kwamba wanahusishwa katika maono ya binadamu wenzao kwa kuwasiliana nao moja kwa moja; maono yanayowapa heshima inayotokana na walimwengu wote kwa jumla; wanyama, mimea na kuwafunza kutilia maanani chochote kisichoelezeka.

Kwa sababu hii, sharti maudhui na mtindo wa kazi hizi uafiki kiwango cha watoto wenyewe kwa kuonyesha ukweli utakaodumu milele, kuwatia moyo watoto na kuwapa imani katika maisha yao. Vitabu hivi vya watoto vihimize ukweli na haki na kwa kufanya hivyo, watoto wataishi vizuri katika kutangamana kwao na binadamu wenzao.