Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kiini cha makosa katika lugha

May 14th, 2019 2 min read

NA MARY WANGARI

BAADHI ya visababishi vya makosa katika lugha ni jinsi ifuatavyo:

Maumbo

Baadhi ya watu katika jamii hupuuza mofu za Kiswahili na kuongea zile zinazopatikana katika lugha mama.

Kwa mfano:

Aliendaga badala ya alienda.

Nipeko badala ya nipe.

Anasomanga badala ya husoma.

 

Wakati mwingine watu huongeza mofu kwenye neno. Kwa mfano:

nipee badala ya nipe

nielekezee badala ya nielekeze

 

Tatizo lingine na linalotokea sana ni pale ambapo watu huonyesha ukubwa na udogo wa majina ya Kiswahili usio wa kawaida.

Mifano:

Katoto badala ya kitoto

Lisaa badala ya saa

Kimtu badala ya jitu

Khatungi badala ya mtungi

 

Kwa sababu ya kuzoea mfumo wa ngeli katika lugha mama, watu wengi hushindwa kuzingatia ngeli za Kiswahili na hivyo kuvuruga upatanisho wa kisarufi. Tazama mifano ifuatayo:

ng’ombe hizi badala ya ng’ombe hawa

mtu mgani badala ya mtu gani

lijitu linene badala ya jitu nene

 

Miundo ya Sentensi

Matatizo katika kiwango cha sentensi aghalabu yanahusu kutozingatiwa kwa uwiano wa kisarufi. Asili ya mwingiliano huu ni lugha mama zisizozingatia mfumo wa ngeli. Mifano:

Makosa                                                        Sahihi

Nyumbani kumekujwa wageni.                    Nyumbani kumekuja wageni.

Mavitu zangu zimeibiwa.                               Vitu vyangu vimeibwa.

Mimi naenda kwa hapo.                                 Mimi naenda hapo.

Tumemalizana?                                               Tumemaliziana?

 

Maana ya Semantiki

Tatizo hili linatokana na hali ya kukosa ufahamu wa kanuni za kisarufi. Vilevile, tatizo hili linahusu kutotambua kati ya viunganishi na vihusishi.

Mifano:

 Alienda na miguu badala ya Alikwenda kwa miguu

 Nilipewa ni baba badala ya Nilipewa na baba

 

Tatizo la Kutafsiri Moja kwa Moja

Mifano:

Anakunywa sigara badala ya Anavuta sigara

Alirudisha ahsante badala ya Alishukuru

kuingiza bao badala  ya kufunga bao

 Nitaandikwa kazi badala ya Nitaajiriwa kazi.

 

[email protected]

Marejeo

Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi, Phoenix Publishers.

Maddo, U. & Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publishers.