Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kongamano la CHAKITA kuanza Alhamisi chuoni Karatina

August 7th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

KONGAMANO la Kimataifa la 21 la Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) litafunguliwa rasmi Alhamisi katika Chuo Kikuu cha Karatina (Bewa Kuu).

Kongamano la CHAKITA ambalo huandaliwa kila mwaka ni maarufu zaidi miongoni mwa wasomi, wataalamu, wapenzi wa Kiswahili na wahadhiri wa vyuo vikuu vyote vya umma na vya kibinafsi kutoka ndani na nje ya Afrika Mashariki.

Ingawa mada kuu ya kongamano la mwaka 2019 ni ‘Kiswahili kwa Maendeleo Endelevu’, zaidi ya wajumbe 200 watakaoshiriki watapania pia kulinganisha mitazamo ya matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali.

Zaidi ya ikisiri 150 zinazohusu taaluma mbalimbali za Kiswahili zilikuwa tayari zimewasilishwa kwa minajili ya kongamano hili kufikia siku ya makataa.

Wajumbe watalenga kutathmini Nafasi ya Kiswahili katika Ustawi wa Ajenda Nne Kuu za Kitaifa pamoja na kujadili Nafasi ya Kiswahili na Ukalimani katika Ujenzi wa Taifa tangu Kiswahili kitambuliwe kuwa Lugha Rasmi ya Kenya katika Katiba Mpya ya 2010.

Kwa mujibu wa Dkt Mark Mosol Kandagor ambaye ni Mwenyekiti wa CHAKITA na Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi mjini Eldoret, washiriki wa kongamano wataweka msisitizo zaidi kuhusu nafasi ya Kiswahili katika ulimwengu wa sasa na haja ya Waswahili wenyewe kuhakikisha kuwa hawawi nyuma katika kuijengea lugha hii nafasi maridhawa kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Washiriki watalizamia pia suala la kuundwa kwa Baraza la Kiswahili nchini Kenya kwa matumaini kwamba hatua hii itapanua wigo na kutoa nafasi kubwa zaidi ya kutangazwa kwa Kiswahili kote ulimwenguni.

Kongamano litahudhuriwa na idadi kubwa ya wajumbe kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Marekani. Kulingana na Dkt Joseph Nyehita Maitaria ambaye ni Katibu Mkuu wa CHAKITA, baadhi ya wageni hawa kutoka mataifa ya nje na sehemu nyinginezo za humu nchini walianza kuwasili katika Chuo Kikuu cha Karatina hapo jana.

Dkt Mussa Hans ambaye kwa sasa ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) anaongoza kundi la wajumbe kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania huku Profesa Pacifique Malonga akiwa kati ya washiriki wanaotazamiwa kutoka Rwanda.

Kongamano litanogeshwa na uwepo wa Profesa Ken Walibora (Chuo Kikuu cha Riara), Profesa Nathan Oyori Ogechi (Chuo Kikuu cha Moi), Profesa Iribemwangi (Chuo Kikuu cha Nairobi), Mwenyekiti wa Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu nchini Kenya Profesa Chacha Nyaigotti-Chacha na Katibu Mkuu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) Profesa Kenneth Inyani Simala kutoka Zanzibar.

Mwandishi Prof Ken Walibora akihutubia washiriki wakati wa kongamano la CHAKITA Agosti 23, 2013, katika ukumbi mmojawapo katika Chuo Kikuu cha Katoliki Afrika Mashariki (CUEA). Picha/ Maktaba

Kundi la wajumbe kutoka Uganda litakuwa chini ya usimamizi na uelekezi wa Dkt Idah Mutenyo wa Chuo Kikuu cha Kabale na Dkt Caroline Asiimwe wa Chuo Kikuu cha Makerere.

Miongoni mwa washiriki kutoka Amerika ambao kufikia sasa wamethibitisha kuhudhuria kongamano hili ni Profesa Samuel Mukoma wa Chuo Kikuu cha Stanford, California, Bw G. Osoro na Bw Jacob Mwita wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kibabii, Profesa Isaac Ipara Odeo atawasilisha makala kuhusu Mchango wa Kiswahili katika Makuzi ya Vyuo Vikuu huku Profesa Clara Momanyi akiwasilisha Makala Elekezi ya kongamano.

Upekee

Akizungumza na Taifa Leo mnamo Jumatatu, Dkt Kandagor alifichua baadhi ya mambo ambayo kulingana naye, yatalifanya kongamano la CHAKITA mwaka 2019 kuwa na upekee zaidi.

“Litawaleta pamoja wakufunzi wa Kiswahili, watafiti, wanafunzi, wanahabari, wasanii, wanaharakati, wanafasihi, wachapishaji, wakereketwa na wadau wa Kiswahili kutoka janibu mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka wizara za michezo, masuala ya vijana, utamaduni na turathi za kitaifa,” akasema Dkt Kandagor.

Ni katika kongamano hili ambapo pia vitabu vitatu vipya vitazinduliwa. Itakuwa mara ya kwanza kwa idadi kubwa zaidi ya vitabu kuzinduliwa kwa pamoja katika historia ya makongamano yote ya awali ya CHAKITA.

“Tutazindua kitabu chenye makala yote yaliyowasilishwa na washiriki wa Kongamano la 19 la CHAKITA lililoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Kibabii, Kaunti ya Bungoma mnamo 2017,” akasema Kandagaor.

“Wingi wa makala zilizowasilishwa katika Kongamano la 20 la CHAKITA katika Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret mwaka jana ulizalisha machapisho mawili ambayo pia yatazinduliwa Karatina,” akaongeza.

Baadhi ya makala za kongamano hilo la Eldoret zimechapishwa katika kitabu Lugha na Fasihi katika Mshikamano wa Kitaifa na Uwiano Barani Afrika na makala nyinginezo kujumuishwa katika Juzuu Maalumu la Jarida la Mwanga wa Lugha ambalo ni chapisho mahsusi la Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi.

Juzuu hili lilihaririwa kwa pamoja na Dkt Samuel Obuchi, Profesa Miriam Mwita na Dkt Noordin Mwanakombo.

Dkt Maitaria anatambua upekee wa mchango wa Chuo Kikuu cha Karatina chini ya uongozi wa Makamu Mkuu, Profesa Muchai Muchiri na wadau wote wa Kiswahili katika kufanikisha mchakato na shughuli za maandalizi ya kongamano la CHAKITA mwaka huu.

“Ndugu zangu wapenzi wa Kiswahili, siku ya kongamano la CHAKITA katika Chuo Kikuu cha Karatina “Wawili-Wawili” imewadia. Waandalizi mpaka sasa wamejitahidi na wanaendelea kujituma sana. Hapa Karatina tumepanga mengi, ni ‘nenda kule, leta hiki, toa kile’. Ukumbi umepambwa tayari kumeza na hata kutema wajumbe wa CHAKITA 2019,” akatanguliza Dkt Maitaria.

Akaongeza: “Wageni waheshimiwa wamealikwa na wamekubali kuhudhuria. Nimezikagua hoteli na zinakidhi hadhi ya wataalamu wa Kiswahili. Kunazo nzuri, nzuri zaidi, bora na bora zaidi! Chaguo ni lako! Tuje sote “Wawili-Wawili” kama kawaida. Hata ukiwa ni “Mmoja-Mmoja” unakaribishwa kwa sababu Mmoja+Mmoja = Wawili! Ukifika hapa umefika, kwingine ni wapi?”