Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kuzungumza au kuwaza kwa haraka na kubadili msimbo

May 14th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

Kuzungumza au kuwaza kwa haraka

AGHALABU mtu anapokuwa na hisia kama vile furaha au hasira, hulazimika kuzungumza kwa haraka haraka na mara nyingi hufanya makosa. Kwa mfano, katika mitihani mtu anapokuwa na muda mfupi kutoa majibu mara nyingi huwa na makosa mengi ya lugha.

Kuchanganya na kubadili msimbo

Hii ni hali ya kutumia aina mbili au zaidi tofauti za lugha katika mazungumzo.

Katika kipengele hiki tunaweza kubainisha aina mbili za kuchanganya msimbo jinsi ifuatavyo:

Kuchanganya msimbo ambapo mzungumzaji hutumia sarufi ya lugha nyingine katika mazungumzo.

Kwa mfano:

nitakukal

unaget

nimereply

Maneno call, get, reply ni misamiati ambayo ni vitenzi vya lugha ya Kiingereza. Kadhalika, nita, una, nime ni mofimu za kisarufi katika lugha ya Kiswahili na zinapata maana zinapopachikwa katika neno.

Mofimu hizi zilipaswa kupachikwa katika msamiati wa Kiswahili na kutuzulia maneno hayo. Aina ya pili ya kuchanganya msimbo ni ile ambao mzungumzaji hutumia maneno kutoka katika lugha mbili au zaidi tofauti katika mazungumzo.

Mifano:-

Ameenda shopping.

Atakwenda church.

Katika mifano hii, vielezi vilivyotumika ni vya lugha ya Kiingereza wakati vitenzi ni vya lugha ya Kiswahili.

Aina ya pili ya msimbo ni ile hali ambayo mzungumzaji anahama kutoka lugha moja hadi nyingine.

Kwa mfano:-

Karibuni wageni. Come and learn with us lugha ya Kiswahili.

Unaenda wapi leo? You are very smart.

What do you want? Sina pesa za kukupa.

Tunaona kuwa katika kila taarifa mzungumzaji anatumia kishazi ama sentensi kamili za lugha katika tungo zake.

“Unaenda wapi leo?’’ na ‘’Sina pesa za kukupa’’ ni tungo kamili zinazochanuza maana inayojitosheleza na zinakubalika kama sentensi sanifu.

Aidha, ‘’Come and learn with us’’, You are very smart’’ na‘’What do you want?’’ni sentensi zinazochanuza maana kamili katika lugha ya Kiingereza.

Aina hii ya msimbo hujulikana kama kubadili msimbo.

 

Sababu ya kuchanganya au kubadili msimbo

Humsaidia mzungumzaji kujieleza vizuri kwa lengo la kufidia upungufu wa msamiati. Upungufu huu unaweza kutokana na mzungumzaji mwenyewe kukosa msamiati wa kutosha au lugha anayoitumia kutokuwa na msamiati wa kutosha.

 

[email protected]

Marejeo

Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.

Maddo, U. & Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publisher.