Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lugha anuwai zinazotumika katika kufanikisha mawasiliano

April 5th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KRIOLI (Creole)

Krioli ni pijini iliyokomaa na kuwa na watu wanaoizungumza kama lugha yao ya kwanza.

Sifa za Krioli ni kama zifuatazo:

Huwa na matumizi mapana kuliko pijini mathalani katika siasa, mziki, vyombovya habari na kadhalika.

Huwa na wenyeji kwa mfano kuna Krioli ya Jamaica, Krioli ya Liberia, Krioli ya Amerika na kadhalika.

Inasheheni msamiati imara unaoweza kutungiwa kamusi.

Huwa na miundo imara ya kisarufi.

Ina matumizi machache ya ishara.

Zifuatazo ni sifa bainifu zinazotofautisha Pijini na Kirioli:

PIJINI KRIOLI
Haina wazungumzaji au wenyeji wazawa

 

Ina wazungumzaji wazawa

 

Huwa na misamiati michache

 

Huwa na misamiati mingi kwa kuwa ni lugha kamili

 

Matumizi yake huwa finyu

 

 Matumizi yake ni mapana

 

Wazungumzaji ni wachache

 

Wazungumzaji ni wengi (kabila)

 

Huwa na miundo hafifu kisarufi

 

Huwa na miundo imara

 

Hutumia ishara kwa wingi kwa sababu ya uhaba wa msamiati

 

Ishara huwa chache kwa sababu kunamsamiati wa ktosha kujieleza

 

Lugha ya taifa

Mipaka kati ya lugha ya taifa na lugha ya kitaifa aghalabu huwakanganya watu wengi. Kwa kukosa kufahamu, baadhi ya watu hutumia dhana hizi mbili kama visawe. Hata hivyo, pana tofauti baina ya dhana hizi mbili.

Lugha ya kitaifa au za kitaifa zinarejelea lugha zote zinazotumiwa na ambazo ni lugha za asili katika taifa fulani. Mfano wa lugha za taifa au lugha asilia nchini Kenya ni kama vile: Kipokomo, Kikalenjin, Kigala, Kimasai, Kikuyu na kadhalika.

Mathalani, lugha ya Kiluo, Kiluhya, Kikalenjin, Kikamba, Kikikuyu na kadhalika.

Hizi ni lugha za kikabila nchini humu kwa kuwa zinasemwa na watu kutoka kabila fulani au wale wanaohusiana na kabila hilo.

Lugha ya taifa nayo ni lugha iliyoteuliwa kama kitambulisho cha utamaduni na ustaarabu wa taifa zima. Ni lugha inayowaunganisha watu kutoka makabila mbalimbali ili waweze kushirikiana na kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya taifa.

Lugha ya taifa inasheheni sifa zifuatazo:

Inafaa kuwa inayovuka mipaka ya kabila fulani ili isiwe lugha ya kikabila.

Inapaswa kuwa lingua franka katika taifa husika. Inapokuwa lingua franca, inakuwa inayozungumzwa na watu wa makabila mbalimbali na wala sio kabila moja pekee.

 

[email protected]

Marejeo

Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O., & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.