Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mambo yanayoathiri mchakato wa kujifunza lugha ya pili au ya kigeni

June 22nd, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MCHAKATO wa kujifunza lugha ya pili hukumbwa na changamoto mbalimbali.

Sehemu kubwa ya mambo hayo ni yale ama yanayomwezesha au yanyoamkwamisha mpataji lugha kupata lugha.

Kwa mujibu wa Martland (1997) mambo hayo ni kama yafuatayo:

Umri

Mtu mwenye umri mdogo ana ahueni zaidi katika kujifunza lugha kuliko mtu ambaye amepevuka kiumri.

Mtoto ambaye hajabaleghe kwa mfano kabla ya miaka tisa ana uwezo wa kujifunza lugha upesi mno. Hali hii inatokana na kwamba mtu mzima tayari anakuwa na lugha nyingine ambayo inasigana na lugha anayojifunza

Hali ya kiuchumi ya anayejifunza lugha

Mtu wa tabaka la chini hawezi kutumia vitu vya kisasa ili kupata lugha. Hii ni kwa kuwa vifaa hivyo ni ghali mno na aghalabu hawezi kumudu bei yake.

Hali ya darasa

Kwa mfano, darasa ambalo limejengewa mazingira ya utani, wanafunzi wanamudu haraka sana kupata lugha. Hii inajumuisha michezo mbalimbali katika darasa hilo.

Msaada wa kifamilia/community support

Ikiwa lugha anayojifunza mwanafunzi inatumika ndani ya jamii hiyo, atapata haraka sana lugha kuliko mwanafunzi ambaye anajifunza lugha ambayo wazungumzaji wake hawako hapo. Kwa mfano, Mtanzania anayetaka kujifunza Kiingereza atapata shida kwa sababu wazungumzaji wake wako nje ya nchi.

Motisha

Ni kipengele muhimu sana katika mchakato wa kujifunza lugha. Kwa mfano, mwanafunzi aliye na motisha ya ndani atapata lugha haraka kuliko anayepata motisha ya nje.

Kiwango cha elimu

Mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu ana uwezo mkubwa sana wa kupata lugha kuliko mtu ambaye hana elimu kabisa.

Matarajio

Ikiwa mjifunzaji lugha ana lengo la kufanya utafiti sehemu fulani, matarajio yake ni kujifunza lugha na kuimudu ili akafanye kazi yake. Kama mwanafunzi hana matarajio yoyote basi itakuwa ngumu kupata lugha.

Haiba

Wanafunzi wacheshi hupata lugha haraka kuliko wanafunzi ambao sio wacheshi. Hii ni kwa sababu watu wachesi hupenda kutagusana sana.

Mtazamo wa utamaduni wa anayejifunza kwa lugha ya pili/kigeni

Endapo mwanafunzi ana mtazamo hasi na lugha anayojifunza basi itakuwa ngumu sana kupata lugha. Mtazamo chanya ndio utakaomsaidia mjifunzaji lugha kupata lugha.

 

[email protected]