Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Manufaa ya kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia

March 23rd, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

HEUGH na wenzake (2007) walibaini kwamba mafanikio yaliyoafikiwa ya wanafunzi kufaulu sana katika masomo ya sayansi na hisabati nchini Ethiopia kati ya 2000 na 2004 yalionyesha tofauti dhahiri. Wanagenzi walipofundishwa kwa lugha ya wenyeji walifaulu zaidi kuliko wale walifundishwa kwa Kiingereza.

Tafiti nyingine sawia zilizofanywa nchini Tanzania na wanaisimu mbalimbali zilitoa matokeo sawa.

Mwinsheikhe (2003) alibaini kwamba wanafunzi wa shule za sekondari waliofundishwa dhana za kisayansi kwa Kiswahili walielewa zaidi na kufanya vizuri zaidi wakilinganishwa na wale waliofundishwa kwa Kiingereza.

Isitoshe, Mwinsheikhe pia anadai kwamba tabia ya kutathmini maarifa ya wanafunzi katika mitihani kwa kutumia lugha wasiyoimudu haifai kwa kuwa hawana uwezo wa kutumia maarifa hayo baada ya mitihani hiyo.

Rubagumya (2003) anatoa hoja kwamba ufundishaji unaotumia lugha inayofahamika baina ya walimu na wanafunzi huleta ufanisi wa kutosha kwa sababu wanafunzi watajua jinsi ya kutumia maarifa ya kidhanifu katika taarifa mpya.

Aidha, Rubagumya anazidi kudai kwamba lugha inapokuwa ni ile iliyozoeleka kwa wanafunzi na ambayo walimu wanaimudu vyema huuleta uelewa mzuri wa dhana ya somo linalofundishwa.

Kwa upnade wake Qorro (1999) anapendekeza kwamba lugha zote mbili zipewe dhima ya kuwa lugha ya kufundishia elimu ya sekondari.

Hata hivyo, hatua hii ina ugumu katika utekelezaji kwa kuwa si rahisi kwa lugha zote kuwa na kazi sawa katika elimu. Badala yake, hatua hii huishia tu kuwachanganya wanagenzi na wakufunzi.

Hivyo basi, tafiti za wanaisimu zinabainisha kwamba, katika mataifa mengi ya Kiafrika, walimu hutarajiwa kuwafundisha wanafunzi kusoma, kuandika na kupata maarifa katika lugha ambayo haikuzoeleka kwa wanafunzi na wao wenyewe.

Walimu wana ujuzi mdogo wa kutumia katika kufundishia.

Idadi kubwa ya tafiti hizo ni za muda mrefu na hazitoi suluhisho kuhusu matatizo yanayowakumba walimu kuhusiana na weledi wa lugha ya kufundishia na ni kipi kinastahili kufanyika ili wanafunzi wapate maarifa yalikusudiwa katika kiwango cha elimu ya sekondari.

Athari ya kutotumia lugha ya Kiswahili katika kufundishia elimu ya sekondari ni kubwa mno.

Walimu na wanafunzi hukabiliwa na matatizo makubwa ya mawasiliano.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Bryman A. (2008). Social Research Methods. London: Oxford University Press.

Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two solitudes assumption in Bilingual education.In J. Cummins & N.H Homberger (Eds),Encyclopedia of Language and Education,2nd Edition,Volume 5.New York:Supringer Science + Business Media LLC.

Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University.