Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia

March 6th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

TUNAANZA kwa kuangazia mada kuhusu Kiswahili kama lugha ya kufundishia.

Hii ni katika kujibu swali kutoka kwa msomaji wetu.

Jina: Martin Mulikuza

Swali: Jadili sera mbalimbali na maoni ya kitaalamu (juu ya) kuhusu matumizi ya lugha na lugha za kufundishia katika nchi ya Tanzania.

Kwanza kabisa, ni vyema tujifahamishe kuhusu dhana ya lugha ya kufundishia.

Lugha ya kufundishia ni lugha mahususi inayoteuliwa na taifa ili kutumika katika shughuli za kutoa elimu rasmi katika nchi taifa.

Ni vyema kuelewa kwamba baadhi ya nchi huwa na lugha zaidi ya moja za kufundishia.

Mfano mzuri ni nchini Tanzania ambapo elimu ya shule za msingi na elimu ya ngumbaru au ukipenda, elimu ya watu wazima huendeshwa kwa lugha ya Kiswahili.

Elimu ya sekondari na ya chuo kikuu hutolewa kwa Kiingereza.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni serikali ya Tanzania imekuwa katika harakati za kuwezesha matumizi ya Kiswahili kama lugha rasmi ya kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini humo.

Kwa upande mwingine, nchini Kenya na Uganda, lugha ya kufundishia ni Kiingereza kuanzia shule za chekechea hadi shule za upili isipokuwa katika baadhi ya masomo.

Taifa la Rwanda nayo ilibadili lugha ya kufundishia kutoka Kifaransa hadi Kiingereza. Nchi nyingi za Ulaya hutumia lugha mame zao kama kama lugha za kufundishia.

Ugumu

Kwa mujibu wa Neke (2003), kuendelea kutumia lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia katika elimu ya sekondari nchini Tanzania ni kuwafanya wanafunzi wa kiwango hiki kuwa na ugumu wa kuelewa kanuni za kisayansi na kiteknolojia kutokana na ujuzi mdogo wa lugha inayotumiwa kufundishia.

Aidha, anaendelea kueleza kuwa baadhi ya walimu wa sekondari hufundisha katika Kiswahili ili kurahisisha somo badala ya kutumia Kiingereza kilichopewa dhima ya kuwa lugha ya kufundishia ingawa mitihani hutungwa katika lugha ya Kiingereza.

Hali hii inadhihirisha kwamba, kutoelewa lugha ya kufundisha kunachangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wanafunzi kushindwa kufaulu katika mitihani.

Baruapepe ya Mwandishi: [email protected]

Marejeo

Bryman A. (2008). Social Research Methods. London: Oxford University Press

Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two solitudes assumption in Bilingual education. In J. Cummins & N.H Homberger (Eds),Encyclopedia of Language and Education, 2nd Edition,Volume 5. New York: Supringer Science + Business Media LLC.

Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University.