Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mbinu za ufundishaji lugha ya Kiswahili

June 6th, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

MBINU za kufundisha Kiswahili ni chungu nzima sawa na jinsi walimu nao walivyo wengi.

Hata hivyo, njia hizi zitategemea hali ya wanafunzi.

Tutajadili baadhi ya njia mwafaka zinazostahili kutumika katika ufundishaji wa lugha ya Kiswahili jinsi ifuatavyo:

Mahojiano

Njia hii haifai kwa mwanafunzi ambaye ni mara yake ya kwanza kusikia Kiswahili.

Hata hivyo, ni mbinu nzuri kwa mwanafunzi ambaye amewahi kusikia habari za Kiswahili.

Kwa mfano, mwalimu anaweza kuandaa maswali na kuwaagiza wanafunzi kuigiza vyeo mbalimbali. Kwa mfano, mmoja wao awe daktari na mwingine awe mwalimu na kadhalika.

Mchezo wa maswali

Kwa mfano, wanafunzi wanaweza kujadili masuala ibuka na muhimu na kisha kuyajibu na katika harakati hizo wanaweza kukusanya msamiati tele wanaoweza kutumia katika nyanja anuwai.

Kwa mfano, lau ungekuwa Rais wa Amerika ungefanyaje kuhakikisha unakomesha ugaidi duniani?

Uigizaji

Katika mbinu hii, mwalimu anahitajika kuwapa wanafunzi mwongozo wa maigizo. Wanafunzi wanaweza kuigiza michezo mbalimbali ikiwemo tamthilia anuwai.

Maswali ya papo kwa hapo (ana kwa ana)

Kwa mfano, Mimi ni Maryamu, je wewe ni nani?

Nyanjani

Nyanjani ni mahali jambo fulani linapotendeka. Kwa mfano, ukitaka kuwafundisha wanafunzi misamiati ya bungeni basi wapeleke bungeni.

Kutumia mazingira mbalimbali

Kwa mfano, ikiwa mkufunzi angependa kuwafundisha wanagenzi mchezo wa kandanda, basi hana budi kuwapeleka uwanjani.

Usomaji

Mfano ni kusoma pande nne za dunia, kuwapa wanafunzi matini mbalimbali.

Majadiliano funge

Hapa wanafunzi hujadili vitu ambavyo vimewekewa mipaka.

 

Je, umeipenda mada hii? Tuandikie maoni au wasiliana na mwandishi: [email protected]

Marejeo

Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi, Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.

Maddo, U. & Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publisher.