Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mbinu za usawiri wa wahusika

June 26th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

WAMITILA (2002) anaeleza kwamba mwandishi au msanii anaweza kutumia njia kadhaa na tofauti katika kuwasawiri wahusika wake.

Huu unaitwa uhuru wa msanii unaomwezesha mwandishi kutumia aina mbalimbali ya wahusika ikiwemo kuteua jinsi ya kuwawasilisha wahusika hao.

Wasomi na wahakiki wa fasihi hutegemea sifa kadhaa wanapowachambua wahusika na kuelezea sifa zao ikiwa ni pamoja na: lugha yao, tabia na mienendo yao,uhusiano wao na wahusika wengine, vionjo vyao, hisia zao kwao na wengine, mandhari na mazingira yao, kiwango cha elimu, jamii na kadhalika.

Katika makala hii, tutaangazia kuhusu mbinu zinazotumika na wahakiki katika kuwaainisha wahusika katika kazi mbalimbali za fasihi.

Kuna mbinu mbalimbali zinazotumika kusawiri na kuwahakiki wahusika ikiwemo: mbinu ya majazi au matumizi ya majina, mbinu ya ulinganuzi na usambamba, mbinu ya matumizi ya wahusika wengine, mbinu ya kimaelezi, mbinu ya kidrama, mbinu ya uzungumzi nafsia.

Mbinu ya Kimaelezi – Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mbinu hii husawiri sifa za mhusika na wakati mwingine hutoa taswira ya maneno, inayomwelezea mhusika anayeangaziwa.

Mbinu hii inapotumika, mwandishi huwa na nafasi ya kubainisha kiwango cha mapenzi au chuki yake dhidi ya wahusika fulani.

Mbinu ya kimaelezi ni njia rahisi ya kuwasawiri wahusika hasa kwa sababu mwandishi anaweza kutoa maelezo machache yanayofumbata wasifu au tabia ya mhusika ambayo ingechukua muda mrefu kutokana na matendo yake mwenyewe.

Udhaifu wa mbinu ya kimaelezi

Mbinu hii huwa haimpi msomaji nafasi ya kushiriki katika kuitathmini tabia ya mhusika anayeangaziwa.

Hii inamaanisha kwamba msomaji hulazimika kuukubali msimamo na kuridhika na maelezo ya mwandishi.

Kwa mfano, “Yasmini alikuwa na kijuso kidogo cha mdawiri mfano wa tungule na macho makubwa ambayo kila wakati yalionekanwa kama yanalengwa lengwa na machozi,”

“Alikuwa na pua ndogo, nyembamba na chini ya pua hiyo ilipangana midomo miwili mizuri iliyokuwa haitulii kwa tabia yake ya kuchekacheka, huku akionyesha safu mbili ya meno yake mazuri. Alikuwa na kichaka cha nywele nyeusi zilizokoza ambazo zilianguka kwa utulivu juu ya mabega yake.

“Alikuwa si mrefu lakini hakuwa mfupi wa kuchusha, na matege aliyokuwa nayo yalizidi kuutia haiba mwendo wake wakati anapotembea” katika riwaya ya Vuta n`kuvute ya Shafi A Shafi (1999).

Maelezo haya ni ufafanuzi wa mwandishi kuhusu mhusika wake katika sehemu ya mwanzo.

Japo hatuelezi waziwazi, ni bayana kuwa uteuzi wake wa maneno unatuelekeza kuamini kuwa ana mtazamo fulani kumhusu mhusika na ambao huenda ukatuelekeza kwenye njia fulani.

 

 

Wasiliana na mwandishi ukitumia baruapepe: [email protected]

Marejeo

Njogu, K. na Chimerra, R. (1999). Ufundishaji wa Fasishi: Nadharia na mbinu. Nairobi- Jomo Kenyatta Foundation.

Syambo, K. Mazrui (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers Ltd