Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Misingi ya uainishaji wa dosari

June 21st, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

UAINISHAJI wa dosari katika ufundishaji wa lugha unaweza kutekelezwa kupitia njia mbalimbali.

Kwa kuzingatia nyanja kuu za lugha jinsi ifuatavyo

Dosari za kifonolojia au ukiushi wa matamshi-lugha ambapo baadhi ya lugha zina toni huku nyingine zikiwa hazina.

Dosari ya kimaumbo au kimsamiati. Hii inahusu mpangilio wa vipashio vinavyounda maneno. Kwa mfano, uwingi wa nomino za Kiingereza hupachikwa mwisho tofauti kabisa na lugha ya Kiswahili ambapo haitabiriki. Vilevile, katika lugha ya Kiswahili neno moja linaweza kuwa na sifa ya kuwa sentensi kwa mfano, “Ninasoma” jambo ambalo kwa Kiingereza haliwezekani kuwa neno moja “ I read”.

Dosari za kimuundo-taratibu; tofauti tofauti zinazotumika kuunda vipashio. Kila lugha ina utaratibu wake. Kwa mfano, My brother- yangu kaka ambapo mfumo huo hauwezekani kuwa sawa.

Dosari za kimaana au kisemantiki – maana huwa ni tofauti tofauti.

Dosari za kipragmatiki- hii ni miktadha mbalimbali kwa mfano sokoni, kanisani.

Uainishaji dosari kulingana na athari za kimawasiliano

Huu ni uainishaji wa dosari kulingana na uelewekaji au kutokueleweka kwa ujumbe uliotolewa na mjifunzaji lugha. Kwa kuzingatia kigezo hiki tunapata aina mbili za dosari.

Dosari za kimalimwengu (global errors) – Hizi ni dosari ambazo zinafanya usemi uliotolewa na mjifunzaji lugha kutoeleweka kabisa

Dosari za kienyeji (local errors) – Hizi ni semi zinazotolewa na anayejifunza lugha ya pili ambazo haziko sahihi lakini zinaeleweka na msikilizaji.

Kwa mfano, “I angry”.

“Ninataka kura” akiwa jikoni au akiwa katika jukwaa anasema: “Ninataka kula”- hizi zinaeleweka na wasikilizaji japo haziko sahihi.

Jinsi ya kushughulikia dosari za wanafunzi

Kila mwanafunzi wa lugha ya pili huwa ana dosari katika kujifunza lugha ya pili. Ni jambo la msingi kushughulikia dosari za wanafunzi, lakini ni muhimu kuzingatia ni wakati gani mwafaka wa kushughulikia dosari hizo kwa kuzingatia muktadha wa darasa ambao unajumuisha mambo anuai kama vile: haiba yao, mihemko, aina ya dosari, umri na kadhalika. Hata hivyo ikiwezekana dosari hizo ziweze kushughulikiwa ili kusaidia zisijirudie rudie.

Baadhi ya wataalamu huona kwamba dosari hazipaswi kushughulikiwa.

Krashen na Terrell(1983), wanasema kwamba mwanafunzi anapaswa aachwe mwenyewe ili azidi kugundua dosari hizo na atazishughulikia mwenyewe.

 

[email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia. Dar es Salaam: BAKITA.

Mulokozi, M. M. (1991). English versus Kiswahili in Tanzania’s Secondary Education. Swahili Studie Ghent