Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Muundo wa andalio la somo

June 22nd, 2019 2 min read

NA MARY WANGARI

UTAYARISHAJI wa somo unatakiwa kuwa na mambo yafuatayo:

Malengo ya jumla (main objectives)

Haya ni mabadiliko ya muda mrefu yanayotakiwa kutokea kwa muda mrefu. Kwa mfano:

  • mwanafunzi aweze kutathmini…
  • mwanafunzi aweze kufahamu…

Malengo haya aghalabu huwa hayabadiliki.

Malengo mahususi /malengo wezeshi

Haya ni malengo ya muda mfupi. Ni malengo ambayo ni ya kudumu lakini shabaha yake ni kusaidia lengo la jumla.

Tofauti kati ya malengo mahusus na malengo ya jumla ni kwamba malengo ya jumla hayapimiki ilhali malengo mahusus yanaweza kupimika.

Malengo mahususi ni mabadiliko ya muda mfupi ilhali malengo ya jumla ni mabadiliko ya muda mrefu.

Kwa mfano:

i. Mwanafunzi aweze kutaja viungo vya binadamu vilivyo katika kichwa.

ii. Mwanafunzi aweze kulinganisha na kulinganua.

iii. Mwanafunzi aweze kuonyesha viungo vya mwili.

iv. Kubainisha viungo vya mwili

Mada kuu

Kila unapoenda kufundisha ni sharti kuwe na mada mahsusi. Mfano wa mada ni Usafiri wa Anga

Mada ndogo

Ikiwa mada yako itakuwa hapo juu, kwa mfano Usafiri wa Anga, mada ndogo inaweza kuwa, kuwasili kwa ndege, kukata tiketi, kufika uwanja wa ndege, mahali uwanja wa ndege ulipo, hali ya miundo mbinu kwenda uwanja wa ndege na mengineyo. Iwapo mada kuu ni familia: basi mada ndogo yaweza kuwa aina za familia

Zaka za kufundishia

Hakuna somo lisilo na zana za kufundishia. Kwa mfano kama ni usafiri wa anga. Unaweza kuchora picha ya jiji fulani, kuwapa ramani na kadhalika.

Utaratibu wa somo/yaani darasani

 

Somo lolote linapaswa kuwa na:

Utangulizi – tanguliza somo lako, kama sio mara ya kwanza wape chemsha bongo, kama ni kwa mara ya kwanza unaweza kuanza na hadithi. Hii itakusaidia kuvuta usikivu wa wanafunzi. Pia unaweza kuwaruhusu wanafunzi wakuulize maswali kuhusu wanachoelewa kuhusu kile unachoenda kukifundisha

Uwasilishaji wa kiini cha somo – unaweza kuandaa maswali, unaweza kuandaa makundi ya wanafunzi wachache wachache.

Utumizi/utendaji wa wanafunzi – Hapa mwalimu anatengeneza mazoezi, kazi binafsi, mazoezi mengine ambayo watafanya wenyewe, maswali ya papo kwa papo au mazungumzo.