Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mwandishi atafaulu zaidi akioanisha fani na maudhui

January 22nd, 2020 3 min read

Na ALEX NGURE

WATAALAMU wengi wamelielezea neno hili fasihi.

Kwa hakika fafanuzi na nadharia juu yake ni nyingi.

Neno fasihi kama linavyoelezewa na wananadharia wote, laonyesha kiwango fulani cha makubaliano kwao kwamba fasihi ni sanaa ya lugha; ingawa zaidi ya hapo, kuna kutokubaliana miongoni mwao. Kutokubaliana huko kwatokana na tofauti zao za kiitikadi, kimtazamo na kimsisitizo. Kuna wale ambao hukazania kwamba fasihi ni ile iliyoandikwa tu.

Lakini sasa inaaminika zaidi kwamba fasihi ni sanaa ya lugha, iwe ya mdomo au uandishi. Kinachohitajiwa kusisitizwa ili kazi fulani iweze kuitwa kazi ya fasihi si jinsi nyenzo za utoaji wake zilivyo (kwa mdomo au kwa maandishi), bali ufundi wa kubeba mawazo katika mbinu za lugha ama ya mdomo au uandishi.

Ukitazama fasihi kwa umbo lake la ndani na umbo lake la nje, utaona kuwa, ni taaluma inayojengwa kwa maneno. Na maneno yenyewe hutumia fani maalumu za aina mbalimbali kutolea dhamira au maudhui ambayo humzingatia binadamu maishani.

Kazi yoyote ya fasihi lazima iwe na sehemu hizi mbili; fani na maudhui. Maudhui ni jumla ya mambo yanayohusiana na yale mwandishi anayokusudia kuyaeleza, na fani ni mbinu ambazo zinatumiwa katika lugha ili kuyaeleza hayo mwandishi aliyokusudia kuyaeleza.

Lakini wananadharia na wataalamu wa fasihi hawatofautiani tu kuhusu fasihi kuwa ni ile ya maandishi au simulizi, bali pia katika suala zima la fani na maudhui. Lipi kati ya mambo haya mawili ni la msingi au linaloongoza katika kuifanya kazi ya fasihi iwe ya fasihi? Kwa baadhi ya wataalamu dhima ya fasihi imo katika kutumbuiza na kuburudisha.

Wengine wanaona dhima inayohusu maisha ya mwanadamu na mwanadamu mwenyewe; hasa katika uhusiano wake na wanadamu wengine na katika mapambano yake na mazingira yake kwa ajili ya maendeleo yake.

Kwa maoni ya wataalam hawa swala la mwanadamu na maendeleo yake, ndilo jambo la mwanzo la kushughulikiwa kabla ya kipengele cha kuburudisha hakijafikiriwa. Lakini pamoja na kujali na kuyapa kipaumbele maswala ya kibinadamu; upande huu wa maoni ya fasihi haudharau haja ya umuhimu wa fani katika fasihi. Kwao pia, fasihi lazima ipendeze na ivutie na kwa hivyo ina kazi ya kuburudisha hatimaye.

Tahakiki

Kambi hizi mbili bila shaka zimekuwa zikitofautiana na kushindana kwenye tahakiki na midani ya kitaalamu. Upande mmoja huona kwamba haifai kusisitiza maudhui, kwani kwa kufanya hivyo mwandishi atainyima kazi yake ule upeo wa juu wa kisanaa.

Pindi maudhui fulani yanayomhusu mwanadamu, maisha na maendeleo yake yataingia kwenye nadhari na hatimaye mikono ya msanii mzuri, atayafinyanga vyema na hatimaye kumfaa anayewasilishiwa kwa nguvu za aina mbili: nguvu za maudhui yenye uzito na nguvu za kisanaa zenye mvuto.

Hali hii humfanya mwandishi wa aina hiyo kuwa mwenye kufaulu zaidi, kuliko yule ambaye ametumia nguvu ya aina moja tu; ya kisanaa au ya kimaudhui zaidi.

S. A. Mohamed anasema: “Kazi ya sanaa hudai iwe na uzuri wenye mvuto wa kisanaa; yaani ipendeze, ivutie au iguse hisia za wasomaji au wale wanaolengwa nayo.

Labda kila msanii anapokuwa anabuni kazi yake, anastahiki kuwa na lengo hili.

Kwa sababu matumizi ya lugha kisanaa hutarajiwa kuwa na uzuri fulani; fasihi kwa hivyo, haihusiani na kuwasilisha mawazo tu, bali kuyawasilisha mawazo hayo kisanaa. Kama msanii atalifikia lengo hili au la, ni jambo ambalo tutawaachia wahakiki.’’

Kwa sababu matumizi ya lugha kisanaa hutarajiwa kuwa na uzuri fulani; fasihi kwa hivyo, haihusiani na kuwasilisha mawazo tu, bali kuyawasilisha mawazo hayo kisanaa. Habari au wazo fulani huweza kuelezwa na kuwasilishwa kwa wasomaji bila kuzingatia haja ya kuwepo usanii wowote ule.

Mara nyingi haja ya mawasiliano katika hali kama hii huishia kwenye lengo la kubeba habari kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Aidha, haja ya mawasiliano yanayoambatana na sanaa huhitaji kuwasiliana kwa mbinu za kimvuto; ile njia inayompa raha au ladha tamu msomaji anapojaribu kuwasiliana na mwandishi wa kazi ya sanaa.

Kwa maneno mengine, ubora wa kazi ya fasihi hutegemea ufundi wa msanii mwenyewe wa kuwasiliana na msomaji; lakini muhimu zaidi, hutegemea anavyojali kuoanisha fani na maudhui.