Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia kuu zinazotumika katika Teknolojia ya lugha ya Kiswahili

February 5th, 2020 3 min read

Na MARY WANGARI

KATIKA kuangazia teknolojia ya lugha kwa Kiswahili, kuna nadharia muhimu zinazotumika kuwapa watafiti na wasomi wa Kiswahili mwongozo.

Miongoni mwa nadharia hizo ni kama vile nadharia ya Msambao wa Ugunduzi na nadharia ya Isimu Kongoo.

Nadharia hizi mbili huchangia pakubwa katika uchunguzi wa teknolojia ya lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya Kiafrika.

Jinsi nadharia hizo zinavyooana na kufidiana

Aidha, nadharia hizi zinawiana na kufidiana mno kwa kuoanisha kipengele cha teknolojia na wakati uo huo kujumuisha kipengele cha uhalisia wa lugha ambayo kama tunavyofahamu, haipatikani katika ombwe tupu, bali miongoni mwa wanajamii.

Nadharia ya Msambao wa Ugunduzi huangazia kipengele cha teknolojia ya lugha kwa mfano jinsi ujuzi wa teknolojia unavyorahisisha mambo katika michakato ya kushughulikia lugha kiteknolojia, utafiti kidijitali tafsiri kimitambo na kadhalika.

Nadharia ya kikongoo kwa upande wake inaleta ukamilifu kwa kuleta upande wa uhalisia ya lugha katika matumizi yake.

Ili kuwa na uelewa mwafaka wa nadharia ya kikongoo ni muhimu kufahamu maana ya kongoo.

Kwa mujibu wa Hurskainen (2005), Kongoo ni mkusanyiko wa matini halisi ya lugha kama ilivyotumiwa katika mazungumzo au maandishi.

Wataalam mbalimbali wametumia nadharia hizi katika tafiti za masuala anuai kuhusu teknolojia ya lugha kwa Kiswahili, utathmini wa matumizi ya teknolojia ya lugha kama vile programu zinazochanganua lugha kisayansi na kijarabati.

Nadharia hizi zinachangia nafasi muhimu katika karne hii ya utandawazi inayohitaji tafiti za kila aina ili kukitosheleza Kiswahili katika nyanja zote kijamii, kiuchumi na hata kisiasa.

Nadharia ya Isimu Kongoo ni maarufu mno miongoni mwa watafiti kutokana na kwamba inajumuisha lugha asilia na vilevile mtazamo wake mpana unaojumuisha nyanja zote za lugha ikiwemo isimu, fasihi, diskosi, isimu jamii na kadhalika kwa kuwa ni mkusanyiko wa lugha asilia

Tayari tafiti mbalimbali za wataalam zimeonyesha jinsi Kiswahili kilivyo kifua mbele miongoni mwa lugha za Kiafrika huku ikipatikana hata mitandaoni, hivyo basi ina nafasi murwa ya kutafitiwa kwa kutumia teknolojia ya lugha, kauli inayoungwa mkono na Muhirwe (2007).

Hoja za wanaisimu kuhusu nadharia za teknolojia ya lugha

Huku akiunga mkono kauli ya Hurskainen (2005), mwanaisimu Muhirwe (2007) anapendekeza mikakati ya kushirikisha lugha za Kiafrika kikiwemo Kiswahili katika utafiti wa kutumia zana na majukwaa ya kikompyuta.

Kwa upande wake Hurskainen (1992), ambaye ni mwasisi wa mradi wa SALAMA, anasema kuwa hamu ya kutumia teknolojia ya lugha katika utafiti na ufundishaji wa lugha za Kiafrika inazidi kuongezeka.

Kando na kudhihirisha kwamba lugha za Kiafrika zikiongozwa na Kiswahili zinaafiki kwa kila hali kutafitiwa kidijitali kwa kutumia teknolojia ya lugha, mtaalamu huyu pia alionyesha hatua muhimu zilizopigwa na watafiti waliotangulia.

Miaka ya 1980 na 1990

Kulingana naye, juhudi nyingi zinazohusu Isimu Kiteknolojia zilisisitizwa na kuelekezwa katika miradi ya kuunda programu za tafsiri kimitambo pamoja na programu za kuchambua lugha kisintaksia.

Aidha, alieleza kwamba lugha za Kiafrika ziliwapa watafiti changamoto za kutosha katika uainishaji wa aina za maneno huku akitoa mfano wa jinsi lugha za kibantu zilifaa kujaribisha programu za kuchambua lugha kimofolojia kwa kuwa zina viambishi na minyambuliko mingi.

Isitoshe, Hurskainen (1999) alifafanua jinsi hazina ya lugha ya Kiswahili katika datakanzi ilivyosaidia kubuni data ya telnolojia ya lugha kwa Kiswahili kwa urahisi na ufasaha hasa wakati maneno yalikuwa yameainishwa kimofolojia, kisemantiki na kisintaksia.

Kulingana naye,mfumo huo ulifaa sana katika uundaji wa programu za utafiti na matumizi ya kawaida kama kuunda kamusi na kukagua tahajia ya lugha ya Kiswahili.

Naye Mabeya (2009) akimnukuu Sewangi (2002), amefafanua kwamba, matumizi mapana zaidi pamoja na lengo la msingi ni kuhifadhi data na kurahisisha mchakato wa uchambuzi wake.

Kongoo matini (text corpus) hutumika kama hifadhi ya lugha katika tarakilishi ili iweze kuchanganuliwa kwa malengo mbalimbali ya kiutafiti kama anavyohoji Mabeya.

Jinsi tulivyoona katika makala iliyotangulia, mradi wa SALAMA unasheheni programu za Kiswahili zinazojumuisha kongoo matini na ya kukagua makosa ya hijai almaarufu kikagua tahajia (spell checker) yenye zaidi ya maneno milioni kumi na mbili ya Helsinki Corpus of Swahili (HCS).

 

[email protected]