Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya Msambao wa Ugunduzi, Nadharia ya Kikongoo katika Teknolojia ya lugha

January 18th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

KATIKA kuangazia teknolojia ya lugha kwa Kiswahili, kuna nadharia muhimu zinazotumika kuwapa watafiti na wasomi wa Kiswahili mwongozo.

Miongoni mwa nadharia hizo ni kama vile Nadharia ya Msambao wa Ugunduzi na Nadharia ya Isimu Kongoo.

Nadharia hizi mbili huchangia pakubwa katika uchunguzi wa teknolojia ya lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya Kiafrika.

Jinsi nadharia hizo zinavyooana na kufidiana

Aidha, nadharia hizi zinawiana na kufidiana mno kwa kuoanisha kipengele cha teknolojia na wakati uo huo kujumuisha kipengele cha uhalisia wa lugha ambayo kama tunavyofahamu, haipatikani katika ombwe tupu, bali miongoni mwa wanajamii.

Nadharia ya Msambao wa Ugunduzi huangazia kipengele cha teknolojia ya lugha kwa mfano jinsi ujuzi wa teknolojia unavyorahisisha mambo katika michakato ya kushughulikia lugha kiteknolojia, utafiti kidijitali, tafsiri kimitambo na kadhalika.

Nadharia ya Kikongoo kwa upande wake inaleta ukamilifu kwa kuleta upande wa uhalisia wa lugha katika matumizi yake.

Ili kuwa na uelewa mwafaka wa Nadharia ya Kikongoo, ni muhimu kufahamu maana ya kongoo.

Kwa mujibu wa Hurskainen (2005), kongoo ni mkusanyiko wa matini halisi ya lugha kama ilivyotumiwa katika mazungumzo au maandishi.

Wataalam mbalimbali wametumia nadharia hizi katika tafiti za masuala anuai kuhusu teknolojia ya lugha kwa Kiswahili, utathmini wa matumizi ya teknolojia ya lugha kama vile programu zinazochanganua lugha kisayansi na kijarabati.

Nadharia hizi zinachangia nafasi muhimu katika karne hii ya utandawazi inayohitaji tafiti za kila aina ili kukitosheleza Kiswahili katika nyanja zote kijamii, kiuchumi na hata kisiasa.

Nadharia ya Isimu Kongoo ni maarufu mno miongoni mwa watafiti kutokana na kwamba inajumuisha lugha asilia na vilevile mtazamo wake mpana unaojumuisha nyanja zote za lugha ikiwemo isimu, fasihi, diskosi, isimu jamii na kadhalika kwa kuwa ni mkusanyiko wa lugha asilia

Tayari tafiti mbalimbali za wataalam zimeonyesha jinsi Kiswahili kilivyo kifua mbele miongoni mwa lugha za Kiafrika huku ikipatikana hata mitandaoni, hivyo basi ina nafasi murwa ya kutafitiwa kwa kutumia teknolojia ya lugha, kauli inayoungwa mkono na Muhirwe (2007).

 

[email protected]

Marejeo

Ashford, R. (2001). Technology and the Potential Spread of Kiswahili. Katika Mdee, J.S. na Mwansoko, H.J.M., Makala ya kongamano la kimataifa KISWAHILI 2000 Proceedings. Dar-es-Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, pp 144-157

Hurskainen, A. (2005). Kiswahili na hali Halisi katika Teknolojia ya Lugha, katika Madumula, J.S na Kihore, Y.M (wah) Toleo Maalumu la Jubilei Miaka 75 ya TUKI (1930-2005) Juzuu-68. Kiswahili- Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

Rass, Theresa (2010). Corpus Linguistics: An introduction to the field and its Use in Linguistics.