Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya Semiotiki

February 27th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

Neno semiotiki limetokana na mnyambuliko wa neno la Kigiriki ‘semeion’ lenye maana ya ishara na linalowakilisha vikundi vya wafuasi wa mielekeo fulani kulingana na maelezo ya John Selden.

Kwa upande mwingine Wamitila anapambanua kwamba ‘semiotiki’ ni neno la lugha ya Kiyunani lenye maana ya ishara na ambalo linatumiwa kuelezea mielekeo ya makundi fulani ya Uhakiki.

Wamitila anakubaliana na Selden kuhusu asili ya neno semiotiki kwa kuwarejelea wasomi Bailey, Matejk na Steiner walioeleza kuwa semiotiki ni mchakato ambapo vitu na matukio huja kutambuliwa kama ishara na kiumbe hai ambacho kinahisi.

Kulingana na Selden, semiotiki ni taaluma ambayo hufanya kazi kwenye desturi pana za kiutamaduni zinazohusisha ishara violwa na ishara tajwa.

Anapozungumzia semiotiki ya kisasa anasema kuwa inatumiwa kurejelea uwanja unaoendelea kubadilika wa elimu ya masomo ambayo huangaza fenomena ya maana katika jamii.

Kulingana na mwanafalsafa wa Kiitalia Umberto Eco, semiotiki inahusishwa na kila kitu kinachoweza kuchukuliwa kuwa ishara.

Nadharia ya Semiotiki ikiwemo matawi na vipera vyake

Wataalamu na waandishi mbalimbali wameweza kutoa mawazo yao tofauti tofauti katika jitihada za kufasiri dhana ya semiotiki.

Kwa mujibu wa Massamba, semiotiki ni taaluma ya kisayansi inayojishughulisha na uchunguzi na uchanganuzi wa mifumo ya ishara mbalimbali ikiwa inazingatia zaidi uhusiano baina ya kiwakilishi na kiwakilishwa.

Kwa upande wao Wafula na Njogu, semiotiki inapambanuliwa kama taaluma ya mipangilio ya ishara zinazomwezesha binadamu kuona vitu au hali kama ishara zenye maana. Kulingana na maelezo ya wataalamu hawa, semiotiki hushughulikia maswala ya ishara, matumizi ya ishara na matumizi ya lugha kwa jumla katika kazi za kifasihi.

Wataalamu hawa wanaeleza kwamba semiotiki huzungumzia uashiriaji wa vipashio vya lugha au tamathali ilhali nadharia ya umuundo inahusu namna ishara zinavyowekwa katika utaratibu unaoziwezesha kufahamika.

Mwalimu Wamitila naye akifasiri semiotiki anasema ni aina ya nadharia ya kimuundo inayojishughulisha na ishara na maana za ishara hizo katika kazi za kifasihi.

Semiotiki huangazia uashiriaji na jinsi kazi za kifasihi zinavyowasiliana na wasomaji. Nadharia hii aidha huchunguza kwa nini kazi za kifasihi zina maana zilizo nazo kwa wasomaji wa kazi hizo. Kwa ujumla, semiotiki ni mfumo wa ishara ambazo zinawakilisha kitu au maana fulani.

Nadharia ya semiotiki imegawika katika matawi tofauti tofauti. Kwa mujibu wa mwanafalsafa Nauta, kuna matawi matatu makuu ya semiotiki ambayo ni kama yafuatayo:

  1. semiotiki fafanuzi
  2. semiotiki tekelezi
  3. semiotiki halisi

Semiotiki ya wanyama (zuolojia)

Hili ni tawi la nne la semiotiki linalotokana na utafiti wa Umberto Eco. Tawi hili ndilo kiwango cha chini kabisa.

Kundi hili linahusu tabia za kimawasiliano za viumbe visivyo binadamu.

Hitimisho

Makundi haya manne makuu ya semiotiki yamegawanywa katika vipera vifuatavyo:

Semiotiki kisintaksia  – Hili ni kundi ambalo  linahusiana na uhusiano wa ishara katika miundo rasmi ya vipengele vya kifasihi.

Semiotiki pragmatiki – Hili ni kundi la pili linalohusiana na ishara na athari zake kwa wanaozitumia.

Semiotiki semantiki – Hili ni kundi linalohusiana na ishara na maana ya vitu inavyorejelea.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus.

Wa Thiong’o, Ngugi (1998). Penpoints Gunpoints and Dreams. Oxford: Clarendon.

Wellek Rene & Austin Warren ( 1986). Theory of Literature. Harmondworth: Penguin