Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya Udhanaishi katika uhakiki wa kazi za Fasihi

March 1st, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

NADHARIA ya udhanaishi inatambua uhuru wa watu wa uchaguzi na hatua ya wazi katika mambo mawili.

Kwa njia tu ya uchaguzi wao wa kuchukua hatua, watu wanaweza kutambua kwamba ni bure, kwa sababu asili ya binadamu ni waliochaguliwa na matendo yao wenyewe kuamua.

Vilevile, nadharia hii huamini katika juhudi za mtu binafsi kujisaka au kupambana na maisha huishia katika mauti.

Inashikilia kuwa maisha ya binadamu yamejaa mateso na pindi tu binadamu anapozaliwa hivyo basi huwa amejipata katika ulimwengu wa mateso na shida hivyo basi kifo tu ndiyo huwa hatima ya kila kitu.

Pia, nadharia hii hujadili hali kama vile mashaka na uchovu wa mambo mbalimbali yanayotutatiza maishani na jinsi yanavyoathiri maisha ya yetu.

Maudhui yanayotajwa na wadhanaishi ni kama vile:

  • uhuru wa mtu binafsi
  • uwezo wake wa kujifikiria na kujifanyia uamuzi

Udhanaishi unafafanua jinsi uhuru wa binadamu umeshikwa na pingu za utamaduni wa jadi mila na itikadi.

Kulingana na wanaoshikilia nadharia hii, ni bora kutambua umuhimu wa kuchagua na kutenda kulingana na uchaguzi na kujitolea majukumu ya maisha.

Isitoshe, nadharia hii pia hujadili na kugusia maudhui ya ukengeushi ambapo binadamu huwa amekata tamaa au amekosa uhakika maishani.

Kutokana na hali hii mwanadamu huwa imembidi kubadilika na kuanza maisha ambayo ni kinyume.

Kwa muhtasari, nadharia hii inarejelea maisha ya binadamu, uhusiano wa binadamu katika ulimwengu na masaibu mbalimbali yanayomkumba.

Kwa mintarafu hii, tunaona kwamba nadharia kama dira ya kuhakiki kazi ya fasihi, pia huwa na dhima ya kuchunguza, kuainisha na kutafiti kazi hizi. Kwa ufupi nadharia hufanya kazi ya fasihi kueleweka vyema. Kwa kuwa fasihi ina dhima kubwa sana katika jamii.

Jinsi tunavyofahamu, fasihi ina nafasi muhimu mno katika jamii katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi.  Dhima ya fasihi katika jamii inajumuisha: kukuza lugha, kukomboa jamii, kukuza utamaduni na kuhifadhi historia ya jamii.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Mulokozi, Mugyabuso & Kahigi K.(1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.

Njogu, K. & R.M. Wafula (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Shihabuddin, C. (1970). Utangulizi. Malenga wa Mvita. Nairobi: Oxford University Press.