Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya utambulisho katika kufafanua michakato ya uteuzi wa lugha

June 26th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

JOHN Weiner (1998), aliyenukuliwa na Wardhaugh, anatumia nadharia ya Utambulisho kuelezea namna mbalimbali za uteuzi wa lugha.

Anafafanua jinsi jamii lugha moja inaweza kuamua ama kutumia lugha kujihusisha na jamii lugha nyingine almaarufu kama makutano au ikatumia lugha kujitenga na jamii lugha nyingine au ukipenda mwachano.

Naye Kihore na wenzake (2009), wanaunga mkono maoni haya ya Wardhaugh pale wanaposema kwamba; makutano ya jamii lugha mbili ni pale ambapo jamii lugha mbili zinapokutana na kuacha kutumia lugha yao na kuanza kutumia lugha ya jamii lugha nyingine.

Hii ni kwa sababu jamii lugha hizi mbili huendelea kutumia hii moja inayodumishwa na kutumiwa kwa utambulisho wa jamii lugha hiyo pana.

Jamii lugha hizi zikiwa na nguvu tofauti, jamii lugha dhaifu hutawaliwa na ile yenye nguvu zaidi.

Hali hii inaonyesha kuwa jamii lugha dhaifu haithamini lugha yake pamoja na utamaduni wake.

Iwapo makutano haya yanahusisha kikundi cha wanajamii ambao wanaacha kutumia lugha yao kabisa ili wajitambulishe na jamii lugha nyingine, hali hii inaweza kusababisha kufa kwa lugha.

Makutano haya yanaweza kuwa yanaelekea juu iwapo mtu anajihusisha na tabia za watu wa tabaka la juu.

Aidha, makutano haya yanaweza kuwa yanaelekea chini iwapo mtu anajihusisha na tabia za watu wa tabaka la chini.

Kwa mujibu wa Giles na Byrne (1982) ambao wamenukuliwa na Kihore na wenzake (2009), wanapambanua sababu anuwai zinazomfanya mzungumzaji wa jamii lugha fulani aamue kutumia lugha ya jamii lugha nyingine kwa utambulisho wake jinsi ifuatavyo:

Utambulisho wa jamii kuonekana kuwa haina umuhimu kwa watumiaji wake.

Mzungumzaji kutoamini kuwa mahusiano kati ya jamii lugha hizi mbili yanaweza kuwa na manufaa kwa jamii lugha yake.

Mzungumzaji kuiona jamii lugha yake ni jamii dhaifu isiyokuwa na maendeleo kwa wanajamii wake.

Mzungumzaji kuiona jamii lugha yake kuwa haina thamani kwa lolote.

Mzungumzaji kujitambulisha kwa jamii lugha yake kwa masuala ya ndani tu, lakini kwa masuala ya maendeleo, elimu na uchumi hujitambulisha kwa jamii lugha nyingine yenye nguvu kwa lengo la kunufaika kijamii na kiuchumi.

 

[email protected]

Marejeo

Kei .K.J. (2002). “Nafasi ya Kiswahili Katika Ujenzi wa jamii Mpya ya Afrika Mashariki”. Nordic Journal of African Studies, ( pp 185-197). West Port, CT: Praeger

Mathooko, M. (2007). Isimu jamii; Misingi na Nadharia. Nairobi: Njogu Books.

Njogu, K & Chimera (1999) Ufundishwa Fasihi : Nadharia na Mbinu.Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.