Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya Uzamaji katika kutatua changamoto za kutumia lugha ya kigeni kufundishia shuleni

April 5th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

WATAALAMU Skutnabb-Kangas na McCarty (2008) wanaeleza uzamaji kama utaratibu wa kurekebisha kasoro za watoto wanaopelekwa shule zenye lugha mbili.

Mpango huu hulenga kuimarisha lugha ya wachache na kuendeleza lugha yao ya nyumbani.

Kwa mfano nchini Tanzania, lugha ya Kiswahili ni lugha ya nyumbani kwa walio wengi, hivyo basi inatakiwa ipewe mikakati ya kuiendeleza kupitia mfumo wa elimu ya Sekondari ambazo zimeenea kote nchini.

Kwa mfano nchini Tanzania, lugha ya Kiswahili ni lugha ya kwanza kwa walio wengi hivyo inatakiwa ipewe mikakati ya kuiendeleza kupitia mfumo wa elimu ya Sekondari.

Lambert (1984) anasema kwamba, elimu ya Utosaji huwakilisha mfumo wa elimu wenye utaratibu uliopangiliwa zaidi kufundishia wanafunzi kupitia lugha ya pili ya wachache.

Kwa upande wake Bostwick (1999), anatoa mifano ya mataifa mathalani Singapore, Uswisi, India, Canada na idadi kubwa ya nchi za Afrika  kama mifano michache ya nchi zinazotambua lugha mbili za taifa. Kwa kawaida, lugha hizi hutumika katika uwanja wa shughuli za kisiasa, kiofisi na kijamii.

Johnson na Swain (1997) wanapendekeza kwamba mtaala wa utosaji unatakiwa uwe sambamba na mtaala wa lugha ya kwanza ya mahali. Hii inamaanisha kuwa mpango wa kuongeza lugha mbili kwa wanafunzi uwe ni kuongeza ujuzi wa lugha ya pili huku wakiendelea kukuza lugha yao ya kwanza na pia utamaduni wa darasa uwe ni jamii lugha ya mahali husika.

Nchini Tanzania kwa mfano, lugha ya Kiswahili ni ya kwanza kwa baadhi na ya pili kwa wengine. Hivyo basi  kuna umuhimu mkubwa wa kutumia lugha ya Kiswahili darasani na lugha ya kigeni kwa madhumuni ya kuongeza ujuzi wa mwanafunzi kimataifa.

Aidha, May (2008) anadai kwamba, lengo kuu la nadharia ya uzamaji ni kuendeleza mwanafunzi kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha ya kufundishia na vilevile kumpa maarifa ya kitaaluma. Cummins (2008) anaeleza kwamba dhana ya uzamaji inatumika kwa mitazamo miwili ifuatayo:

Muktadha wa elimu: Dhana ya uzamaji inatumika kama utaratibu wa mfumo wa kupanga elimu inayofundishwa kwa lugha mbili ambapo wanafunzi huzamishwa katika mazingira ya kujifunza lugha mbili. Lugha ya kwanza ya kufundishia kwa kawaida huanza kwa mwaka wa kwanza au wa pili mwanzoni mwa mpango wa masomo.

Je, una swali au suala lolote ungependa mwandishi aangazie? Tuma kwa: [email protected]

Marejeo

Bryman A. (2008). Social Research Methods. London: Oxford University Press.

Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two solitudes assumption in Bilingual education.In J. Cummins & N.H Homberger (Eds),Encyclopedia of Language and Education,2nd Edition,Volume 5. New York: Springer Science + Business Media LLC.

Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University