Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia za kujifunza lugha

June 12th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

NADHARIA za kujifunza na kufundisha lugha ya pili au lugha ya kigeni huhusisha sifa zifuatazo:

  1. Mbinu ya tafsiri sauti
  2. Mbinu ya moja kwa moja (direct method)
  3. Mbinu ya usomaji (reading approach)
  4. Kusikia na kusimulia (audiolingual method)
  5. Kushirikisha jamii (community language learning method)
  6. Mbinu ya ukimya (silence method)
  7. Mbinu ya mawasiliano (communicative language approach)
  8. Mbinu ya mwitiko jumuishi(total physical response)
  9. Mbinu ya utambuzi (communitive code method)
  10. Mbinu ya upendekezi (suggestopidia method)

 

Mbinu ya tafsiri sarufi/ mbinu ya kimapokeo

Mbinu hii huhusisha mkabala ambapo ufundishaji wa lugha ya kigeni hujiegemeza katika sarufi ya lugha ya Kilatini.

Waasisi wa mbinu hii ni Meidinger (1783) na Ploetz (1849).

Iliasisiwa katika enzi ambapo lugha ya Kilatini iliaminika kuwa ndiyo lugha bora zaidi.

Nafasi ya lugha mama ilipuuzwa kwa kiasi kikubwa na ilijikita katika sarufi ya Kilatini.

Hivyo basi, mwalimu alipaswa kujikita katika kufundisha sarufi ya Kilatini na vipengele vingine vilipuuzwa.

Mbinu ya tafsiri ilihusisha mkabala elekezi kwa maana ya kwamba mkufunzi anawaelekeza watu kuhusu namna ya kutumia lugha na sivyo wanajamii wanavyotumia lugha husika.

Mbinu ya moja kwa moja (direct method)

Mwasisi wa mbinu hii ni mtaalamu Gouin (1880).

Nadharia hii inazingatia uzungumzaji wa lugha husika. Mbinu zilizopaswa kufundishia ni zile zilizohamasisha wanafunzi kuzungumza. Kwa mfano, mbinu ya majadiliano, uigizaji, maswali katika vikundi na kadhalika.

Masomo yalianza kwa hadithi fupi halafu wanafunzi wangeuliza maswali kuhusu hadithi waliyosimuliwa huku mwalimu akiwaambia watoe maoni yao kuhusu hadithi hiyo.

Matumizi ya vielelezo yalitumika zaidi kwa mfano vielelezo kama picha, ramani, katuni na mengineyo.

Kipengele cha sarufi kilifungushwa kwa kufuata muktadha halisi ambamo lugha inatumika. Kipengele cha utamaduni kilifundishwa kwa uchache sana.

Mbinu ya usomaji (Reading approach)

Mbinu hii inatumika kufundishia wanafunzi wanaojifunza lugha ya kigeni na ambao hawatarajiwi kutoka nje ya nchi ambapo lugha hiyo inatumika.

Madhumuni yake huwa kuendeleza uwezo wao wa kusoma ile lugha. Vipengele vinavyofundishwa ni vile vinavyohusu usomaji kwa hivyo vipengele vingine havihusiki.

Msisitizo wake ni kwamba anayejifunza lugha aweze kusoma vitu vingi kwa wakati mmoja. Mbinu hii haimpi mwanafunzi wa lugha uwezo wa kuzungumza lugha husika bali ni kuisoma tu.

 

[email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318.

Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia. Dar es Salaam: Matbaa ya Ghent