Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia za kujifunza na kufundisha lugha

June 6th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

Nadharia ya utabia (Behaviourism)

MWASISI wa nadharia hii ni B. Watson.

Wataalamu wengineo wanaoafikiana na nadharia hii ni pamoja na Leornard Bloomfied, O.N Mowrer, B.F. Skinner na A.W. Staats.

Edward Thorndike (1935), alikuwa wa kwanza kabisa kutafiti zaidi.

Kwa mujibu wa wataalamu wanoaegemea nadharia ya utabia, mtu kujifunza lugha ni mwigo kwa maana ya kwamba anaiga kile kinachosemwa na watu wanaomzunguka.

Burrhus Frederic Skinner pia alitafiti zaidi kuhusu nadharia ya ujifunzaji. Kulingana naye ni kwamba anaafikiana na dhana ya mwigo mwigo lakini anaongeza kuwa ni uimarikaji wa tabia. Hii inamaanisha kwamba hivyo mtoto mdogo hazaliwi na lugha bali huichota kutoka kwa wazazi wake.

Naye Wilga Rivers (1968), anasema mtoto hujifunza kupitia kujaribu na kukosea ‘trial and error’ na huendelea kufanya hivyo mpaka anapofikia matamshi ya jamii nzima.

Vidokezo muhimu kuhusu nadharia hii ni kwamba:

Nadharia hii huyapa mazingira nafasi kubwa katika mchakato wa mtu kujifunza lugha.

Inazua swala nyeti, je, mtu akitengwa na jamii anaweza kuwa na lugha?

 

Nadharia ya utambuzi

Mwasisi wa nadharia hii ni mwanaisimu Jean Piaget (1954).

Kwa mujibu wa mtaalamu huyu, kuna kipindi maalum cha kupata lugha binadamu anapozaliwa.

Jean alidai kuwa shughuli ya kujifunza lugha ni sehemu ya ukuaji wa binadamu kwa maana kwamba kadri unavyokua ndivyo unavyozidi kupata na kuelewa lugha. Anazidi kufafanua kwamba mtoto hupata lugha kabla ya kuzaliwa.

Kwa upande wake, Arth(2003), anadai kuwa mtoto hupata na kuelewa lugha kabla ya kuzaliwa kuanzia miezi 0-18.

Nadharia hii haipingani na umuhimu wa mazingira katika ujifunzaji lugha.

 

Nadharia ya uumbaji

Mwasisi wa nadharia hii ni Jerome Brunner.

Hoja kuu ya nadharia hii inasisitiza nafasi ya mama katika upataji lugha ya kwanza.

Mtoto hutengeneza lugha kutegemea na mawasiliano ambayo mama yake anayatumia.

Brunner alidai kwamba ili mtoto aweze kupata lugha ni lazima mambo yafuatayo yatimizwe:

  1. Muktadha
  2. Tajriba (experience)
  3. Upangilifu (organisation)
  4. Kujenga mazingira ya upekuzi (udadisi)

Je, umeipenda mada hii? Tuandikie maoni au wasiliana na mwandishi: [email protected]

Marejeo

Chiraghdin, S. & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, J.C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers.