Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi na mchango wa lugha katika jamii

March 2nd, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

LEO tunaendeleza mada kuhusu uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii katika Kiswahili.

Tutaendeleza mada hiyo kwa kuichambua na kuitathmini kwa njia ifuatavyo: Lugha huwezesha watu wa jamii fulani kupata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya jamii.

Isitoshe, kulingana na Austin (1962), ni muhimu kuhusisha matumizi ya lugha na muktadha wake wa kijamii kwa kuwa lugha huwa na matumizi tofauti kama kutoa mapendekezo, kuahidi, kukaribisha, kuomba, kuonya, kufahamisha, kuagiza, kukashifu, kusifu, katika uapisho na kadhalika.

Lugha ndicho chombo kinachotumika kuwaleta pamoja na kuwaunganisha wanajamii huku ikisaidia kuimarisha uhusiano miongoni mwa wanajamii.

Katika muktadha wa Kiafrika kwa mfano, heshima ya mtu inatambulishwa na jamii ya watu ndiyo maana Waswahili wana msemo unaosema “mtu ni watu”.

Kwa jumla, kauli hii inatuonyesha kuwa katika harakati za maisha za wanajamii, heshima na kukubalika kwa mtu pamoja na kueleweka kwake kunatokana na namna mtu anavyohusiana na wanajamii wengine pamoja na mambo mengine ikiwa ni kutumia lugha kwa ufasaha.

Haya yote yanawasilishwa kutoka katika jamii moja kwenda katika jamii nyingine kwa kutumia lugha ambacho ndicho chombo muhimu cha mawasiliano.

Jamii hutambulika kwa kutumia lugha. Lugha huwa na uwezo wa kuonyesha sifa fulani kuhusu mzungumzaji anayerejelewa na uhusiano uliopo kati ya wanajamii. Utamaduni hutambulishwa katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu kwa kutumia lugha. Kwa mfano, katika fasihi ya kabila la Wahaya, tunatambua mambo mbali mbali yanayohusu kabila hili hasa katika kipengele cha majigambo kutokana na namna wanajamii hawa wanavyotumia lugha yao kujipambanua kwa jamii nyingine.

Lugha pia hutumika katika kurithisha mila na desturi za jamii ikiwa ni pamoja na kutolea elimu.

Binadamu huweza kufunzwa na kupewa maadili mbalimbali kwa kutumia lugha ili waweze kujitambua kuwa wao ni akina nani na wapo ulimwenguni kwa malengo gani.

Kwa mfano, watoto huweza kufunzwa masuala yanayohusu uana wao ambao hutokana na jinsia yao kwa kutumia lugha.

Pamoja na kuwa wanajamii wanaona matendo yanayotendwa na jamii nyingine au ndani ya jamii hiyo lakini wanahitaji namna ya kuambiwa juu ya uzuri au ubaya wa matendo hayo, kufuata au kutoyafuata ambapo lugha huchukua nafasi yake.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Halliday, M. A. K. (2003). On Language and Linguistics. (Jonathan Webster Ed.) Continuum International Publishers.

Masamba, D. (2004). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ipara, I. O., & Maina, G. (2008). Fani ya Isimujamii kwa Shule za Sekondari. Nairobi: Oxford University Press (OUP).