Habari Mseto

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya hisia katika uboreshaji kazi ya Fasihi Andishi

November 15th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

USHAHIDI unathibitisha kwamba riwaya nyingi zinajihusisha na aina moja kuu ya hisia; yaani ya kuona tu, na pengine kusikia.

Kwa kawaida, mwandishi huandika kuhusu yale anayoyaishi kuona, kusikia, kuonja, kunusa au kuhisi katika maisha yake ya humu duniani. Hivyo, ni dhahiri kwamba mwandishi ataathiriwa na mazingira ya alipozaliwa, kukua na hata mastakimu yake ya kawaida.

Waandishi waliokulia vijijini aghalabu huwapeleka wahusika wao vijijini, na wale waliokulia mijini huwapeleka mijini kupitia maandishi yao. Hata William Shakespeare aliathiriwa na mambo kama haya katika nyingi za tungo zake. Waandishi wa riwaya za Kiswahili wameshindwa kabisa kuelezea mazingira wanayoyajua kwa kutumia hisia zote tano au hata zaidi.

Kwa mfano, Kitabu ‘Sifi Mara Mbili’ chake Nicco ye Mbajo kinazungumzia maisha na mazingira ya kijijini kabla ya Maneromango kuhamia mjini. Lakini hakuna tafauti yoyote ya wazi inayobainisha ushamba na maisha ya mjini katika riwaya hii. Ndivyo ilivyo katika riwaya nyingine nyingi tu kama vile Ukitoa Siri Utachinjwa na Mauaji ya Lojing’i (J.M Simbamwene) kwa kutaja chache tu. Mwandishi anao uhuru wa kuchagua mandhari na wapi pa kuwapeleka wahusika wake.

Iwe mjini au mashambani, hakuna udhuru wa kutotumia hisia nyingi au zote tano. Hakika, mwandishi wa riwaya ana uwanja mpana zaidi wa kuranda akitumia silaha kali ya kalamu na maneno. Riwaya ina upana na urefu wa kumwezesha mwandishi kujifaragua, hasa katika majitapo ya wahusika, nafasi ya mazingira na urefu wake. Kila sehemu ina mazingira yake ambayo kwayo mwandishi anaweza kuranda na kujifaragua.

Shambani kuna mashamba, mjini kuna maghorofa; shamba kuna mito, mjini kuna mitaro; shambani kuna harufu ya maua, mijini harufu ya uturi, taka, na kadhalika. Kwa bahati mbaya, kama ilivyo katika riwaya, mashairi mengi yanazungumzia hisia ya kusikia zaidi na pengine kuona.

Matunda

Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa kazi maarufu kama vile ‘Sauti ya Dhiki’ na ‘Malenga wa Mvita’. Mathalani hata yale mashairi mwanana ‘Jana na Leo na Kesho’ na ‘Zindukani’ yanaelezea hisia hizo mbili tu: kuona na kusikia! Hakuna haja ya kutoa mifano ya mashairi mengine mengi katika magazeti ambayo aghalabu si ya viwango vya chini kisanii tu, bali hata kimaudhui.

Kwa upande mwingine, mfano mzuri wa shairi ambalo limesheheni hisia nyingi ni ‘Kufua Moyo’ la Sheikh Shaaban Bin Robert ambalo lina hisia za kuona, kugusa na kunusa.

Ukiondoa ‘Mashetani’, hali nayo ni vivyo hivyo katika takriban tamthiliya zote nyinginezo. Bali kuna juhudi ambazo zinaanza kutoa matunda, ingawa haieleweki kama jitihada hizi ni za kukusudia au ni ajali tu. ‘Isinyago & Midimu’ ni tamthiliya ambayo inafungua ukurasa mpya mintaarafu ya suala hili la hisia.

Kuna haja kubwa ya waandishi kuzichunguza jamii zao kwa makini, wapenye katika nafsi za wahusika na mazingira yao ambayo ni muhimu mno ili kuwaelewa wahusika wenyewe pamoja na kuleta maana na taswira kamili ya kisa kinachoelezwa.

Zana

Maneno ni zana ya pekee inayoweza kumkaribisha au kumtenga mwandishi na wasomaji wake. Kutokana nayo, anaweza kuelezea hisia nyingi ambazo zitamfanya awe kipenzi, mcheshi na pengine hata mkombozi wa wasomaji. Si lazima hisia zote ziwekwe au kuelezewa pamoja, kwani hivyo ni kushurutisha; na ni kinyume cha mambo. Kinachosisitizwa ni kuwa hisia mbalimbali zionekane katika kazi nzima kwa jumla ili kuipa ubora na sura ya juu.

Said A. Mohamed anasema kwamba uandishi ni kazi ngumu, lakini ni kazi ya hiari pia. Ugumu wake ni kama sabaganga, una kazi nyingi ndani ya moja. La muhimu ni idili na saburi. Chambilecho Abdilatif Abdallah:

Mambo yataka busara, kinguvunguvu hayendi,

Yataka tuvu fikira, nyotu sizo na mapindi,

Fikira za kitwa bora, kitwa bupu hakiundi.

Kila hisia ina umuhimu wake kutokana na mazingira ya tukio linalohusika au kusimuliwa. Maana kazi zote za sanaa hutokana na matendo na maisha ya watu ambao katika matukio, visa na mazingira yao hutumia hisia zao zote tano ama kwa pamoja au kwa nyakati mbalimbali.

Ili basi msomaji aweze kupata mandhari kamili, na hata yeye mwenyewe ashiriki katika matukio yenyewe kwa kuchukia, kuonea huruma, nk; ni muhimu, kabla ya yote, apate hisia zote hizo tano. Kazi ya sanaa inayojihusisha na hisia moja tu au mbili huwa muflisi kisanii kwa vile inashindwa kuwasilisha mandhari za hali halisi kwa msomaji.

Je, mara ngapi nyoyo zetu husononeka au kuripukwa kwa maya kwa sababu ya sauti ndogo tu ya ndege aliaye pekee nyikani, au nyimbo ya zamani?

Sauti ya ndege huweza kuleta majonzi ya miaka mingi mno ya utotoni wakati ambapo mtu alifiwa na mzazi, ndugu, jamaa au sahibu wake. Kadhalika, nyimbo za kale huweza kuchimbua ashiki ya zamani baina ya wapenzi, au kutonesha jeraha la masaibu na madhila yaliyopita. Na wala si nyimbo na sauti ya ndege tu, pengine hata harufu ya maua huwa na nguvu za kumbukumbu kubwa mno.