Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya Kiswahili kama lugha rasmi na ya taifa

November 12th, 2019 3 min read

Na ALEX NGURE

LUGHA ya taifa ni lugha inayotumika katika taifa fulani kwa shughuli za kitaifa kama vile mikutano ya kisiasa.

Kimsingi, ni lugha inayoleta mshikamano wa kitaifa.

Aghalabu hutumiwa kwa utambulisho wa kitaifa mbali na kazi ya msingi ya mawasiliano. Kwa mujibu wa Prof J Habwe na wenzake (2010), Lugha ya taifa ni lugha inayotumiwa kuwaleta pamoja watu wenye historia na asili moja, au makundi ya watu wamoja waliofungamana na kuwa na tabia na nyendo ambazo zina manufaa kwa wote. Katika Kenya na Tanzania, Kiswahili ni lugha ya taifa na rasmi vilevile.

Chiraghdin (1977), Fishman (1968), Eastman(2001) na Greenfeld (2001) wanazifafanua dhana za taifa na utaifa kama mfumo na mpangilio wa makundi ya watu wamoja waliofungamana na kuwa na tabia na nyendo ambazo huwatofautisha na watu wengine.

Aidha, taifa na utaifa huwahusu watu na ada zao; watu na itikadi zao; watu na mila na desturi zao; katika maingiliano ya kibinadamu kama vile arusi, matanga, jando na unyago n.k. au watu wenye lugha maalum na fasihi inayofungamana na mawazo ya watu hao, matumaini yao na utu wao.

Lugha rasmi ni ile inayotumiwa katika kuendesha shughuli za kiserikali ambazo ni rasmi, mathalani, kufundishia shuleni, biashara baina ya taifa na mataifa ya kigeni, uandishi wa sheria n.k.

Lengo la lugha rasmi si kuunganisha watu kama ilivyo katika matumizi ya lugha ya taifa, bali ni kuhakikisha shughuli fulani imefanywa kwa urasmi.

Kutokea miaka ya themanini, Kiswahili kimepata msukumo na umaarufu mkubwa nchini Kenya, Afrika Mashariki na Kati na ulimwenguni kote. Mabadiliko katika mfumo wa elimu yamekifanya Kiswahili kuwa somo la lazima katika shule za msingi na upili. Isitoshe, kuna ongezeko kubwa la vyuo vikuu vinavyofundisha somo la Kiswahili. Mashindano ya nyimbo, michezo ya kuigiza na mashairi kwa shule za msingi, upili na vyuo yamekiimarisha Kiswahili pakubwa.

Wataalamu wengi wa Kiswahili wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Bunge linabuni sera ya lugha na Baraza la Lugha la Taifa-Kenya (BALUTA)- mithili ya Baraza la Kiswahili la Taifa-Tanzania(BAKITA), ambalo litakuwa mratibu wa kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili.

Hata hiyo, licha ya ufanisi mkubwa ambao Kiswahili kimepata kama lugha ya taifa, bado kingali kinakumbwa na changamoto nyingi. Baadhi yazo ni:

Hatua ya Kenya kukiteua Kiswahili kuwa lugha ya taifa na pia lugha rasmi sambamba na Kiingereza ingali kuzaa matunda. Hatua hii haina budi kuungwa mkono kikamilifu na mfumo wa siasa na nadharia-endelezi za Kiswahili.

Kiingereza na lugha nyingine za kigeni zingali zinachukuliwa kuwa ndiyo lugha za hadhi na za kumpatia mtu kipato kizuri, na hivyo kupewa kipaumbele shuleni zaidi ya Kiswahili. Baadhi ya watu wangali wanakihusisha Kiswahili na tabaka la watu wa kisomo duni au wasio na kisomo chochote. Si ajabu basi, hata baadhi ya wabunge wanaotoka katika maeneo ambayo ndiyo chimbuko na kitovu cha Kiswahili, wanakionea haya Kiswahili.Hawatoi hoja zao kwa Kiswahili bungeni.

Kiswahili bungeni

Ndiposa Mohamed Ali almaarufu Jicho Pevu na wengine katika bunge la taifa na seneti wanaotoa hoja zao na kuwasilisha miswada bungeni kwa lugha ya Kiswahili wanastahili kongole. Shikilieni hapo hapo Waheshimiwa.

Hivi majuzi, Spika wa bunge la Tanzania alitoa changamoto kwa wabunge wa Kenya kutumia Kiswahili bungeni. Spika huyo aliwashauri wabunge hawa: ‘Mkiamua kuongea kwa Kiswahili ongeeni kwa ufasaha; mkiamua kuongea kwa Kiingereza ongeeni kwa ufasaha’

Mchango wa vyombo vyetu vya habari; redio, runinga na magazeti, katika kuikuza lugha ya Kiswahili tunautambua. Hata hivyo, kuna kasumba ya watu wengi hasa wasimamizi wa baadhi ya vyombo hivyo kuamini kwamba masuala ya kitaaluma si muhimu kujadiliwa kwa Kiswahili katika vyombo vya habari. Kwa hakika, wasikilizaji na watazamaji wanaoongea Kiswahili wanahiniwa wakati ambapo mijadala mingi yenye umuhimu wa kitaifa inapoendeshwa kwa Kiingereza.

Baadhi ya vyombo hivyo vya habari vimekuwa vikikubalia Kiswahili kutumika kama lugha ya mizaha isiyozingatia kanuni za sarufi na lugha kwa ujumla. Shirika la NMG linastahili pongezi kwa kuwa msitari wa mbele katika kuiendeleza lugha hii kupitia Taifa Leo; gazeti la Kiswahili linalotekeleza wajibu usio kifani. Tunahitaji magazeti zaidi ya Kiswahili nchini Kenya.

 

[email protected]