Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia Afrika Mashariki

March 13th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KULINGANA na mjadala wetu wa awali, ni bayana kwamba ili mwanafunzi apate maarifa na uwezo wa kujitambua na kung’amua kile kilichofundishwa na mwalimu wake ni sharti awe na umilisi wa lugha ya kufundishia.

Mekacha (2000) anaunga mkono hoja hii kwa madai kuwa, watu hufikiri katika lugha na lugha hutumika katika kufikiri.

Lugha ndiyo nyenzo ya kuwasilisha na kuweka wazi fikra na mawazo.

Kutokana na hali hii ni wazi kuwa lugha na kufikiri ni mambo yanayofungamana.

 Aidha, Mekacha anahoji kwamba“Lugha na kufikiri ni mambo yaliyofungamana mno kiasi kwamba haiwezekani Kujadili mojawapo bila kulihusisha na jingine. Kusema kuna hudumia fikra na fikra hujibainisha katika kusema.

Kwa mintarafu hii, ni dhahiri kuwa lugha ya kufundishia inatakiwa iwe ndiyo inayowezesha mwanafunzi kufikiri na kuamua ni kipi anachostahili kusema kwa wakati ulio sahihi.

Kwa upande wake Prah (2003), anafafanua kwamba lugha ya kwanza ikitumika kama lugha ya kufundishia huwezesha watu kujiamini.

Hii inadhihirisha kuwa lugha ya kufundishia ina dhima kubwa katika maendeleo ya jamii kwa kukuza fikra pevu ambazo ni msingi wa ubunifu na ugunduzi.

Isitoshe,  Prah anaendelea kudai kwamba lugha ya kufundishia ndiyo inayotumika kujenga mfumo wa elimu na ndiyo lugha inayotumiwa kuwasilisha stadi na maarifa ya msingi ya umma na ndiyo ya kuimarisha ubunifu na kuendeleza maarifa ya wale wanaojifunza.

Hivyo basi, huwa ndiyo lugha ya kulimbikiza na kuhifadhi maarifa.

Kwa mujibu wa Tikolo (2012), ufahamu wa mwanafunzi wa lugha aliyoizoea wakati wa kukua kwake inaweza kuwa ndiyo msingi wa ujifunzaji mzuri wa baadaye, pale anapounganisha na ujuzi wa mwalimu wake.

Kwa upande wake Rubanza (2002), wanafunzi wa Tanzania hupoteza ujuzi wa Kiingereza mara tu wanapohitimu elimu yao.

Hii ni kwa sababu jamii inayowazunguka haitumii lugha ya Kiingereza, hivyo kupoteza lugha hiyo baada ya muda mfupi wa kumaliza elimu ya sekondari.

Kulingana na Vuzo (2002), lugha ya kufundishia inaweza kuathiri uwezo wa ujifunzaji kufafanua maelekezo na maswali.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Kothari, C. R. (2004). Research methodology: Methods and Technique (Second Revised Edition). New Delhi: New age International Publishers.

Koul L. (2009). Methodology of Educational Research (4th ed.). New Delhi: Inda Vikas publishing House PVT Ltd.

Lambert, W et al (1960). “Evaluational Reactions to Spoken Languages”. Journal of Abnormal and Social Psychology. 20.1